TANZANIA HAIWEZI KUWEPO BILA YA MUUNGANO, TUULINDE KWA WIVU- DKT. TULIA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa ni wajibu wa kila mtanzania kuhakikisha anailinda kwa wivu wote tunu ya Muungano iliyoanzishwa na waasisi wa taifa hilo.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 25 Aprili 2025 wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Pwani wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika stendi ya Kibaha ikiwa ni sehemu ya shughuli za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanyika katika mkoa huo.


Kiupekee, Dkt. Tulia amemshukuru na kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha anasimamia maendeleo katika nyanda zote za bara na visiwani.
“Tanzania haiwezi kuwepo bila Muungano, Muungano huu umejengwa katika misingi imara umedumu na utaendelea kudumu. Kila mmoja wetu anapaswa kutafakari matendo na maneno yake yawe chachu ya kudumisha Muungano wetu, niwahakikishie kwamba Bunge litaendelea kuwa daraja katika pande zote mbili ili kuhakikisha Muungano unazidi kuwa madhubuti, unadumu na kuwa imara zaidi” Amesisitiza Dkt. Tulia