REA YAHAMASISHA FURSA YA MKOPO UJENZI WA VITUO VIDOGO VYA BIDHAA ZA MAFUTA VIJIJINI

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kuwahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa ya mikopo kwa ajili ya kuwezesha ujenzi na uendeshaji wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta ya Petroli na Dizeli kwa maeneo ya vijijini.
Hayo yamebainishwa na Mhandisi Mwandamizi Deusdedit Malulu wa REA, jijini Dar es Salaam katika Warsha na wadau wa sekta ya uuzaji wa biashara ya mafuta na chama cha wamiliki wa Vituo vya mafuta vya rejareja nchini (TAPSOA).
“Tumekutana na wafanyabiashara wa mafuta ili kuwaeleza fursa ya mikopo inayotolewa na REA ili kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijiini ambayo itachochea ukuaji wa uchumi katika maeneo hayo.


Vile vile, tumewapatia washiriki walijitokeza katika warsha hii mwongozo unaosimamia utoaji wa mkopo huu pamoja na fomu ya maombi ya mkopo husika ili waweze kuomba fursa hii,”
Mha. Malulu amewaeleza kuwa, Serikali itaendelea kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo hususan vituo vipya vidogo vya gharama nafuu maeneo ya vijijini ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya mafuta kwa gharama nafuu, kwa njia salama, na isiyo na madhara kwa mazingira.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika warsha hiyo, TAPSOA wameishukuru REA kwa kuitisha warsha ambayo imekua chachu katika kuhamasisha matumizi bora ya nishati vijijini na kuiomba REA kuendelea kutoa ushirikiano ili kuifanya sekta ya bidhaa ya mafuta kuwa mkombozi katika kujenga uchumi wa wananchi na kuhifadhi mazingira.
TAPSOA ni chama cha wamiliki wa Vituo vya mafuta vya rejareja nchini ambapo kupitia warsha hiyo, fursa hii imetambulishwa kwao ili kuwezesha ushiriki wao na kuifanya sekta ya mafuta kuwa na tija nchini hususan katika maeneo ya vijijini.