MTANZANIA DKT. DEO MWAPINGA ACHAGULIWA KUWA KATIBU MKUU WA FP-ICGLR

Katika mafanikio makubwa ya diplomasia ya Tanzania na ushirikiano wa kikanda, Mtanzania Dk. Deo Mwapinga ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Jukwaa la Wabunge wa Nchi Wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR). Anachukua jukumu hili kufuatia kuidhinishwa kwa kauli moja na Maspika wa Mabunge wa Nchi nchi wanachama wa ICGLR.
Uidhinishaji wa Dk. Mwapinga baada ya kuteuliwa na Maspika wa ICGLR umefanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa FP-ICGLR uliofanyika Luanda Angola leo Aprili 25, 2025 ambapo Wabunge wanaowakilisha mabunge ya Ukanda wa Maziwa Makuu walikutana kujadili masuala ya amani, usalama na utawala wa kidemokrasia ikiwa ni pamoja na kupitishwa kwa uamuzi wa Maspika kuhusu Uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa FP-ICR.

Katika hotuba yake ya kukubalika nafasi hiyo, Dk Mwapinga alitoa shukrani kwa nchi wanachama kwa heshima hiyo, na kuahidi kudumisha Malengo ya FP-ICGLR na kuimarisha ushirikiano wa wabunge katika ukanda wa maziwa Makuu.
“Hii sio tu heshima kwangu bali uthibitisho wa imani kubwa Nchi wananchama wa ICGRL walionayo kwa Tanzania hususani katika kupambania maswala ya ulinzi na amani, ushirikiano wa kikanda na maswala ya demokrasia. Ninakubali jukumu hili kwa ufahamu kamili wa kazi na umuhimu ulio mbele yetu, ambao ni kupigania amani na usalama, kuimarisha diplomasia ya kibunge, kukuza ushirikiano wa kikanda, na kukuza demokrasia, na utawala bora katika eneo letu.” Alisema Dkt. Deo.
Jukwa la Bunge la ICGLR linajumuisha Mabunge kutoka nchi 12 wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu likiwa na lengo la kusaidia utekelezaji wa itifaki iliyosainiwa mwaka 2006 katika kuimarisha, Ulinzi na Usalama, demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.
Akiwa Katibu Mkuu, Dk. Mwapinga atakuwa na jukumu la kuratibu programu na shughuli za kongamano hilo lenye makao makuu yake Mjini Kinshasa Kongo, ambapo pamoja na mambo mengine ni pamoja na, kuimarisha mazungumzo baina ya mabunge, na kuhamasisha uungwaji mkono kwa malengo muhimu ya maendeleo ya kanda.
Dk. Mwapinga alipata uungwaji mkono wa kishindo kutoka kwa Maspika wanaowakilisha Nchi zao katika Mkutano wa 15 wa Jukwaa la Mabunge ya Ukanda wa Maziwa Makuu – ICGLR ulionza tarehe 20 hadi 25 April 2025 , jambo linalodhihirisha wazi imani kubwa walionayo Nchi wanachama wa ICGRL kwa Tanzania.
Nafasi ya Katibu Mkuu mpya wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR) ilikuwa ikiwaniwa na nchi tatu wanachama ambazo ni Burundi, Kenya na Tanzania ambapo uamuzi ulitolewa na Maspika wote wa ICGRL kwamba Tanzania inastahili nafasi hii kuongoza ajenda za ICGRL kwa miaka mitatu ijayo ikiwa na kipengele cha kuongezwa muhula mwingine mara moja baada ya Kenya na Burundi kujitoa katika kugombea.
Serikali ya Tanzania imeupokea kwa furaha uchaguzi huo huku Naibu Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azzan Zungu ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania nchini Angola akiutaja kuwa ni wakati wa kujivunia kwa nchi yetu kuwa na diplomasia imara katika Kanda wa Maziwa Makuu na ni ushuhuda wa uongozi wetu katika masuala ya kikanda unaosimamiwa na vyema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt Mwapinga anamrithi Mhe. Balozi Onyango Kakoba kutoka Uganda ambaye alitumikia nafasi hiyo tangu Machi 2018. Mhe. Kakoba ni Mbunge wa zamani wa jimbo la Buikwe Kaskazini mwa Uganda. Pia alichukua nafasi hiyo kufuatia uteuzi wa Maspika na muda wake kumalizika Oktoba 2024.
Uteuzi huo unaashiria sura ya kihistoria si kwa Tanzania pekee bali kwa Nchi wanachama wa ICGRL kwani inatafsiri uongozi mpya wa Tanzania katika kusukuma agenda zilizopo katika Jukwaa hili.
Akizungumza baada ya Ushindi huo Mhe. Elibarick Kingu (Mb) ambaye aliongoza kampeni kwa kufanya mazungumzo na Wabunge wa Nchi Wanachama wa IFGLR kwenye mkutano huo kuomba kuungwa mkono huko Luanda Angola anasema “Huu ni ushindi wa Bunge la Tanzania na Nchi kwa Ujumla kwa Mtanzania aliyechaguliwa na pia ni faida ya kimkakati kwa Tanzania kwa ujumla. Hatua hii inaiweka nchi yetu katika ramani ya maamuzi katika moja ya taasisi nyeti sana katika ukanda huu umuhimu wa kijiografia barani Afrika,” alisema.
Mhe. Kingu ambaye ni mzoefu katika na maswala ya kidiplomasia na ushawishi, aliteuliwa na Spika wa Bunge Mhe. Tulia Ackson (Mb) kuongeza nguvu katika ujumbe wa Tanzania uliokuwa ukimpigia debe Dk.Deo Mwapinga kwenye kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.
Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR) lilianzishwa tarehe 4 Desemba 2008, mjini Kigali, Rwanda na Wakuu wa Nchi za ICGLR na jukwaa hilo lina jukumu muhimu katika kuhakikisha kwamba vyombo vya kutunga sheria vya nchi wanachama vinashiriki kikamilifu katika mchakato wa amani na ulinzi ikiwa ni pamoja na maendeleo wa kikanda.
Pia ni jukwaa linalowezesha ushirikishwaji mzuri wa wabunge katika utekelezaji wa malengo ya ICGLR ya kusimamia Kukuza Amani na Usalama, Kuendeleza Demokrasia na Utawala Bora, Kuimarisha Ushirikiano wa Kikanda, na Kushughulikia Maendeleo ya Uchumi na Usimamizi wa Maliasili.
Mapema akitoa ufafanuzi kuhusu uchaguzi huu Mjumbe wa Kamati Tendaji ya FP-ICGLR kutoka Tanzania Mhe. Eng. Ezra Chiwelesa (Mp) ameukaribisha uteuzi wa Dkt. Deo kwa furaha na kuutaja kuwa ni maendeleo chanya kwa diplomasia yetu ya Kibunge kupitia uongozi wa Mhe. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Muungano wa Mawaziri.
“Uchaguzi huu unadhihirisha nia thabiti na uwezo wa Spika wetu Mhe. Dk. Tulia Ackson (Mb) ya kuimarisha diplomasia na ushirikiano wa Kibunge katika Ukanda wa Maziwa Makuu kwa kufanya mazungumzo na Maspika kutoka Nchi Wanachama ili kuiunga mkono Tanzania katika nafasi hii. Chini ya uongozi mpya wa Dk. Deo Mwapinga, tunaamini Jukwaa hili litakua na nguvu zaidi katika kushughulikia masuala ya Amani na Usalama, demokrasia, Uwazi na Utawala wa Sheria,” alisema Mhe. Ezra Chiwelesa