WAZIRI MAVUNDE AELEKEZA KUPITIWA UPYA UTARATIBU WA MALIPO YA MRABAHA KWA MADINI YA METALI

0
IMG-20250423-WA0048


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa kuanzia tarehe 1 Julai, 2025, mfumo wa ulipaji mrahaba (royalty) kwa wachimbaji wa madini ya metali (base metals) kwa biashara ya ndani ya nchi utabadilika ambapo sasa utatozwa mahali madini yanapopokelewa badala ya mahali yanapotoka, hususan madini yanayopelekwa viwandani katika hatua inayolenga kuongeza tija kwa wachimbaji wa madini hayo sambamba na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Hatua hiyo ni sehemu ya Serikali kupitia Wizara ya Madini kuendelea kuonesha dhamira ya dhati katika kuimarisha Sekta ya Madini kwa kuweka mkazo katika kuwawezesha wachimbaji wadogo kukua hadi kufikia kiwango cha kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa.

Mhe. Mavunde ameyasema hayo leo Aprili 23, 2024 wakati wa kikao maalum na Viongozi wa Tanzania Base Metals Association (TBMA) jijini Dodoma kujadili masuala nyeti ya sekta hiyo.

Waziri Mavunde amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuendelea kuhamasisha watanzania wengi kujihusisha na shughuli za madini kwa kuwatengenezea mazingira mazuri na hatimaye kuchimba kwa tija na kuongeza vipato vyao sambamba na kuongeza manufaa ya sekta katika uchumi wa taifa.

Mhe. Mavunde amemuelekeza Kamishna wa Madini kuhakikisha anaandaa utaratibu maalum wa kushirikiana kwa karibu kati ya wizara na taasisi nyingine kama TRA,NEMC nk kuhakikisha mchimbaji mdogo anapata huduma yoyote kutoka Serikalini kwa urahisi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesema kuwa pamoja na hatua hiyo, Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuwainua wachimbaji hao ikiwa ni pamoja na kuimarisha utafiti wa madini kupitia dira ya Vision 2030 ambapo serikali inalenga kuongeza kiwango cha utafiti wa madini kutoka asilimia 16 hadi 50 ifikapo mwaka 2030.

Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza kuhusu zuio la usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza thamani ya madini hapa nchini kabla ya kuyasafirisha nje.

“Tunataka madini yaongezewe thamani hapa nchini, tuzalishe ajira, tuongeze mapato na mwisho wa siku tuwafikishe wachimbaji wadogo katika hatua ya mafanikio ya kweli.

Kwa yale madini ambayo bado hatuna teknolojia ya kuyachakata nchini,serikali itaangalia namna bora ya kuwezesha uchimbaji huo pasipo kuathiri matakwa ya sheria kwa kusaidia upatikanaji wa masoko ya ndani ya nchi”amesisitiza Mhe. Mavunde.

Sekta ya madini inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa taifa, ambako mchango wake katika Pato la Taifa umefikia asilimia 10.1 kwa mwaka 2024. Jitihada hizi zinaonesha wazi kuwa serikali ipo makini kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *