ULEGA AONGOZA WADAU KUCHANGIA BIL. 1.6 KUFANIKISHA KONGAMANO LA eLEARNING AFRICA

0
IMG-20250417-WA0011

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega akimwakilisha  Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amewaongoza wadau wa sekta ya elimu kuchangia harambee ili kufanikisha  Kongamano la Kimataifa la eLearning litakaloangazia Teknolojia za Kidigitali sekta ya  elimu linalotarajia kufanyika Mei 7-9, 2025  katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Katika harambee hiyo Wizara ya Elimu inatafuta shilingi bilioni 1.6 ili kufanikisha kongamano hilo la 18 Barani Afrika  ambapo kwa mwaka huu linatarajiwa kuleta washiriki 1,500 pamoja na mawaziri wa elimu zaidi ya  50 kutoka Nchi mbalimbali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuchangia harambee hiyo,  Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema kuwa hakuna namna Tanzania kukwepa matumizi ya TEHAMA na teknolojia mbalimbali katika mifumo ya utoaji elimu bali ni kuhakikisha wanaenda pamoja  na maendeleo hayo.

Mhe. Ulega amesema  kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hilo kunatokana na ukweli kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amieweka nchi katika ramani kupitia uimarishaji wa Diplomasia ya kimataifa, hatua hiyo imechochea ukuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukuza bunifu na teknolojia  ikiwemo matumizi ya TEHAMA  katika elimu.

Prof. Mkenda amesema kuwa kupitia kongamano hilo wadau zaidi ya 1,500 wakiwemo Mawaziri wa Elimu kutoka Nchi zaidi ya 50 watashiriki kujadiliana mwelekeo katika nyanja mbalimbali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa kongamano hilo linaandaliwa na Tanzania kwa kushirikiano na Taasisi ya eLearining Afrika.

Prof. Nombo amesema kuwa Tanzania wanatarajia kunufaika na fursa mbalimbali kupitia kongamano hilo ikiwemo kubaini mikakati na mbinu za kuongeza matumizi ya Teknolojia katika elimu na sekta nyengine, kuvutia programu za pamoja za uzalishaji bunifu za teknolojia zilizoibuliwa nchini.

Amesema kuwa  pia kuvutia makampuni ya teknolojia ya kimataifa kuja kuwekeza, kuimarisha ubia baina ya sekta ya umma na binafsi katika maendeleo na matumizi ya teknolojia,  digital sekta ya elimu.

“Kongamano linakwenda kuchangia uchumi wa ndani kupitia bidhaa na huduma zitakazotolewa na washiriki wa kongamano na kukuza sekta ya utalii kwa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii” amesema Prof. Nombo.

Katika Kongamano hilo limebeba Kauli mbiu  isemayo : kufikilia upya elimu na maendeleo na Rasilimali Watu kwa Ustawi wa Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *