TAMISEMI YAPONGEZWA NA BENKI YA DUNIA KWA UTEKELEZAJI MZURI UJENZI WA MIUNDOMBINU KUPITIA MRADI WA SEQUIP

Benki ya Dunia imeipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa ujenzi wa shule mpya zilizojengwa kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari SEQUIP ambao umepunguza umbali kwa wanafunzi kufuata elimu suala ambalo lilikuwa likiwakatisha masomo yao hasa jinsia ya kike.
Pongezi hizo zimetolewa na Huma Kidwai Mtaalamu wa Elimu kutoka Benki ya Dunia ambaye ni Mtaratibu wa Mradi wa SEQUIP kwa niaba ya Benki ya Dunia baada ya kutembelea shule ya Sekondari ya Amali ya Katerero iliyoko katika Halmashauri ya Bukoba ambayo imejengwa kupitia mradi huo katika Mkoa wa Kagera.


Akisistiza umahiri wa wanafunzi katika shule hizo mpya, Kidwai amewashauri Wakuu wa shule hizo kujifunza mbinu mpya kwa shule Kongwe na kuwa wabunifu ili kuzalisha wanafunzi bora na mahiri.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mratibu wa Mradi wa SEQUIP Richard Makota amesema shule hizo zilizojengwa zinalenga kuwasaidia wanafunzi kupata elimu kwa vitendo na nadharia kutokana na miundombinu iliyowekwa hasa kwa masomo ya Sayansi.
Aidha, Ferdinand Eladius Mkuu wa shule ya Sekondari ya Amali ya Katerero akizungumza kwa niaba ya walimu wenzake amesema uwepo wa shule hiyo umewasaidia wanafunzi kupenda masomo kutokana na upekee wa miundombinu iliyopo.
