NCC YATOA MBINU KUPUNGUZA GHARAMA ZA UJENZI

0
IMG-20250410-WA0009

Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wa sekta ya ujenzi nchini kwa kutoa mafunzo yatakayowawezesha kutekeleza miradi kwa ufanisi, kupunguza gharama zisizotarajiwa, na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vilivyokusudiwa.

Kupitia mafunzo hayo, NCC imelenga kuwajengea uwezo waajiri, wakandarasi na washauri elekezi kusimamia mabadiliko ya kazi, madai na migogoro kwa njia inayozuia upotevu wa muda, fedha, na rasilimali nyingine hali inayopunguza gharama kwenye miradi ya ujenzi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), miradi ya ujenzi huathiriwa na mabadiliko ya kazi, ucheleweshaji wa kushughulikia madai, na migogoro, ambavyo kwa pamoja husababisha ongezeko la gharama, muda wa mradi na hata kushusha viwango vya ubora.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mhandisi Tumaini Lemunge kutoka NCC amesema, “Lengo letu ni kuona miradi ya ujenzi inatekelezwa kwa gharama zilizopangwa na kwa ubora unaokubalika”

Ameongeza kwa kusema kuwa, Kupitia mafunzo haya, washiriki wamepata mbinu za kupunguza mabadiliko yasiyo ya lazima, kushughulikia madai mapema, na kutatua migogoro kwa mujibu wa mikataba.

Wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi waliopata nafasi ya kushiriki wameeleza namna mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhandisi Lyda Osena kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) amesema “Mafunzo haya yameniongezea uwezo wa kutambua, kuepusha na kusimamia migogoro na madai kwa njia ya kisheria, vilevile yatanisaidia kutekeleza miradi kwa ufanisi zaidi, ndani ya muda, bajeti na ubora uliokusudiwa.”

Mkadiriaji Majenzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ameongeza, “Nimepata uelewa mpya kuhusu umuhimu wa mabadiliko katika mikataba ya ujenzi. Sasa najua kuwa mabadiliko hayawezi kuepukwa kabisa, lakini yanahitaji usimamizi makini ili kuepusha gharama zisizokuwa za lazima.”

Kwa upande wake, Mwanasheria Elizabeth Kimako kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) amesema, “Mwanasheria anaposhiriki katika mchakato wa ujenzi anatakiwa kuelewa kwa kina masuala ya kimkataba. Mafunzo haya yamenipa uelewa wa kusaidia taasisi yangu kuendesha miradi kwa ufanisi”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *