BILIONI 100 KUKARABATI MADARAJA BARABARA YA KUSINI

KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi and Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla amesema serikali imetenga kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja matano kwenye maeneo korofi ya barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kusini.

Makalla ameyasema hayo leo wakati kwenye siku yake ya kwanza ya ziara mkoani Lindi ambapo pamoja na mambo mengine alipita katika Kata ya Somanga Mtama iliyopo katika Jimbo la Kilwa Kaskazini mkoani Lindi kwa ajili ya kusalimia wananchi wa eneo hilo na kujionea mwenyewe maendeleo ya ukarabati wa dharura wa barabara iliyoharibiwa na mvua.
Makalla alizungumza baada ya kupata maelezo mafupi kuhusu maendeleo ya ukarabati wa dharura wa maeneo korofi aliyopewa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aambaye alimkuta katika eneo hilo akiwa anasimamia shughuli zinazoendelea kufanywa na wataalamu wake. Makalla alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu na inajali maisha na maendeleo ya watu na ndiyo sababu imeamua kuwekeza kiasi hicho kwa ajili ya ujenzi wa madaraja hayo muhimu ili kufanya barabara hiyo muhimu ipitike kwa majira yote ya mwaka.

“ Leo nimepita hapa kuja kusalimia wananchi na kujionea mwenyewe maendeleo ya matengenezo ya barabara hii ambayo yaliathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi. Serikali ya Rais Samia itatumia zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kukarabati madaraja hayo,”alisema.
Kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kumpongeza Ulega, watendaji wa TANROADS na watumishi wa wizara ya ujenzi waliohusika na ukarabati kwa kujenga maeneo hayo kwa weledi, kasi kubwa na kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mawasiliano kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Kusini yanarejea.

“Nakupongeza sana ndugu yangu Ulega, kwa weledi mkubwa uliouonyesha kwa kuweza kurudisha mawasiliano hayo kwa muda mfupi na napenda kukwambia kuwa unatakiwa kuwa mkali pale uzembe unapotendeka kwani kile anachokifanya ni kwa maslahi ya CCM kwa sababu ndicho chama chenye dhamana kwa wananchi.
Kabla ya Makalla kuzungumza, Ulega alimpa taarifa fupi ya maendeleo ya ukarabati unaoendelea ambao hata hivyo alisema hautaathiri ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya madaraja katika maeneo korofi ya barabara na kumshukuru Rais Samia, ambaye ni pia ni Mwenyekiti wa CCM, kwa kuhakikisha fedha za kutosha zinatengwa kwa ajili ya kazi hiyo.