REA YAPAMBA MOTO UHAMASISHAJI MATUMIZI YA UMEME

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuhamasisha matumizi sahihi na endelevu ya umeme kwa Watanzania ikiwa ni pamoja na matumizi ya vifaa vya kisasa vya umeme hususan majiko ya umeme ambayo yanatumia kiasi kidogo cha umeme, salama kwa afya za watumiaji na kwa gharama nafuu.
Hayo yamebainishwa na Wataalam wa REA waliofika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kutumia fursa ya miradi ya REA inayotekelezwa mkoani Mara.


Akizungumza katika mkutano na wananchi, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka REA, Abdulrazack Mkomi amesema kuwa, majiko ya umeme yanalinda afya za watumiaji na ni nafuu kulinganisha na matumizi mengine ya nishati ya mkaa na kuni.
Ameongeza kuwa, ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, REA itaendelea kusambaza kwa wingi majiko ya gesi nchini ikiwa ni sehemu ya kuitangaza na kurahisisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Naye, Mhandisi wa Miradi ya REA mkoa wa Mara, Omary Gwillah amesema kuwa, mkoa wa Mara umeendelea kuwahamasisha wananchi kuunganisha umeme kwenye vitongoji baada ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukamilisha utekelezaji wa mradi wa kuunganisha umeme kwenye vijiji vyote nchini.

Mha. Gwillah ameongeza kuwa, Serikali imeweka mkazo katika kusambaza umeme kwa watanzania ili kuwa na maendeleo endelevu pamoja na kujenga uchumi imara na kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu kwa watanzania wote.
“Kufikisha miundombinu ya umeme hadi kwenye vitongoji kumekuwa kipaumbele muhimu katika juhudi za kuboresha uchumi na maisha ya Watanzania. Kupitia uunganishaji umeme, kutachochea ongezeko la viwanda vidogo na vya kati pamoja na kuboresha huduma za afya na elimu,” amesema Mha. Gwillah.