WANASAYANSI WAKUTANA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA

0
IMG-20250402-WA0008

Wabobezi katika sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi wamekutana nchini Tanzania katika kongamano kwa ajili ya kujadili mchango wa kukabiliana masuala mbalimbali ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Kongamano hilo limeratibiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, likijumuisha wataalamu wa sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tasnia zinazohusiana kutoka Tanzania na Afrika Mashariki.

Akifungua kongamano hilo Mwenyekiti wa Bodi ya TMA Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari, amesisitiza ushiriki wa wataalamu wengi kutoka Afrika Mashariki katika mchakato wa IPCC kutoka Afrika Mashariki.

“Ni matumaini yangu kuwa kupitia makongamano kama haya ya uhamasishaji wa wanasayansi kujihusisha katika kufanya tafiti zinazokidhi matakwa ya IPCC, wataalam wengi zaidi kutoka Afrika Mashariki wataweza kutoa mchango kikamilifu katika utayarishaji wa ripoti za tathmini ya Saba ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ya IPCC (IPCC AR7)” amesema Jaji. Mshibe

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa IPCC, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa ripoti za IPCC zimekuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kimataifa na nchi moja moja.

Dkt. Chang’a amesema kuwa ripoti ya IPCC ya AR7 inayoandaliwa inatarajiwa itakuwa na jukumu muhimu katika mustakabali wa hatua za kuchukua dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa natabianchi kwa kuzingatia taarifa za kisayansi.

“Taarifa hizo zitakuwa zimehakikiwa vyema ambapo zina mchango mkubwa katika kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kikanda na Duniani kote,” amesema Dkt. Chang’a.

Kongamano hilo limeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuongeza uelewa kuhusu shughuli za Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Ripoti zitakazoandaliwa katika mzunguko wa saba wa IPCC (AR7) kuhusu tathmini ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na fursa za kushiriki katika mchakato huo.

Mchakato huo ikijumuisha uandishi, uteuzi wa wataalamu na mapitio ya ripoti za IPCC pamoja na kuhamasisha wanasayansi hasa vijana, watendaji, wakufunzi na wanafunzi kufuatilia na kushiriki katika mchakato mzima wa shughuli za IPCC katika mzunguko wa saba ulioanza mwaka 2023 na unatarajiwa kumalizika mwaka 2029 au 2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *