YA CHADEMA NA MWENEZI BAWACHA; USHAHIDI MWINGINE WA UDHAIFU WA LISSU

Alipogombea TLS kuwa Rais watu walionya: huyu mtu ni mwanaharakati na kamwe hajui mifumo ya ujenzi wa taasisi na hatakuwa na muda huo! Hamkusikia.
Vijana wakawa na haraka wakamchagua Tundu Lissu kuwa Rais wa TLS, kilichofuatia ni aibu ya mwaka katika historia ya Chama hicho tangu kianzishwe, imeandikwa historia, atabaki kuwa Rais wa hovyo wa TLS wa wakati wote. Maana hata vikao tu vya Governing Council alikuwa hajui vinaitishwa lini na nani?
Tuwakumbushe tena, hata akiwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, historia ni ile ile Lissu si mjenzi wa mifumo ya taasisi wala uongozi ni mtu anayejua tu kuzodoa, kubeza au kupiga propaganda. Kuna wakati alikuwa anatafutwa kukaa kwenye vikao vya Chama Kanda ile kupitia mikakati anashangaa hivi tunatakiwa tukae, kikao ni limi na cha nini tena😀😀!!
Alipochukua fomu ya kuwania Uenyekiti wa Chadema Taifa tulionya! Hamkusikia. Tulisema bayana mtu huyu hana sifa hata moja ya kuwa Mkuu wa taasisi inayopigania Dola na inayopaswa kuwaunganisha wanachama wake nchi nzima. Narudia hana sifa hata moja! Mkapuuza!
Leo mambo mawili yanaweza kuthibitisha hoja kuwa Chadema inapita katika zama za uongozi dhaifu na usio na mikakati kuliko wakati wowote katika historia ya Chama hicho. Kwa nini?
Mosi, ni kuibuka kwa Lissu na kauli ya kiharakati ya “No Reform, No Election” ambayo asilimia 98 ya Wanachadema hawaelewi ni falsafa ya Chama kwa miaka yake yote ijayo au uchaguzi huu? Na ni falsafa au propaganda? Na kauli hiyo kama ilizingatia maoni ya wagombea ubunge udiwani na nafasi nyingine za uwakilishi?
Matokeo yake Chama hicho, imethibitishwa pasi kuacha shaka, hii leo kiko kwenye mtanziko mkubwa wa ndani kisiasa hasa miongoni mwa wagombea ubunge na udiwani.
Mamia ya wanachama wa chama hicho wanaona Mwenyekiti wao mpya na mwanaharakati isiyezingatia misingi ya sayansi za siasa amekuja na kauli au slogani ya kumtanabaisha yeye mwenyewe kama mwanasiasa-mwanaharakati na si falsafa makini na inayopimika inayoweza kukivusha chama. Vilio na miguno ni mingi ndani ya Chama hicho. Nisikilize mimi!
Pili, sasa hii ndio kubwa kuliko, taarifa kwa umma iliyotolewa leo Machi 31, 2025, na Chadema kuhusu Mwenezi wao wa Baraza la Wanawake Taifa (Bawacha), Sigrada Mligo, aliyepigwa na kuumizwa vibaya nje ya kikao alichokuwa anakisimamia Makamu wa Chama hicho Taifa, John Heche, ni kauli ya hovyo kuwahi kutolewa na Chama cha siasa.
Na hii yote inakwenda kwenye udhaifu wa kitaasisi wa Chadema chini ya Lissu.
Taarifa ile kwanza imekosa ubinadamu kwa majeruhi huyo akiwa kiongozi wa chama Taifa na zaidi inamtisha mgonjwa eti “chama kinafuatilia mienendo yake na mahusiano yake na CCM.”
Kivipi yani? Kisa baadhi ya wanaCCM kwenda kumuona hospitalini au kushinikiza apate haki yake??
Chadema hii hii haikusema “inafuatilia mienendo” ya Tundu Lissu huyu huyu siku wanaCCM na viongozi waandamizi walipomtembelea maeneo mbalimbali iwe nchini, Nairobi au Ubelgiji.
Iko hivi Lissu anajenga ugonjwa mpya ndani ya Chadema kwamba aaminike yeye tu wenzie wote wanaweza kuwa wasaliti. Huwezi wewe kuwa mkamilifu siku zote na wenzio sio wakamilifu siku zote. Haiwezekani.
Lissu kukutana na viongozi wa Serikali na kufanya maridhiano ya kudai alipwe pesa zake za Bungeni ilikuwa ni sawa, Mbowe alipokutana na Serikali kwenye maridhiano ya kuleta “reforms” Lissu huyu huyu aliongoza kampeni chafu ya kubeza maridhiano hayo na kuonesha wenzake ni wasaliti.
Leo yuko katika mtanziko mkubwa: amebeza maridhiano leo anahubiri mabadiliko ambayo hawezi kuyapata bila maridhiano. Kabaki anapuyanga! Anakiuza Chama na kukiingiza mkenge kwa kukosa maono!
Tanbihi yangu ni kwamba kumtisha mgonjwa aliyeko wodini akipigania afya yake kisa anatembelewa na watu mbalimbali wawe wa Chadema au CCM ni ushuhuda wa mapema sana wa kwamba uongozi wa mkurupukaji Tundu Lissu umekosa mwelekeo, ni dhaifu na hautakaa utoke kwenye tope hilo.
Tulionya na nasema tutaendelea kuonya Chadema ijinasue chini ya Lissu hakuna na wasitarajie “leadership” yoyote ya maana zaidi yataongezeka mateso ndani ya chama hicho, usaliti na kukosa mwelekeo.
Alamsiki.
Niite Mwamba, Mwamba, Mwamba wa Kaskazini.