COMMONWEALTH YARIDHIA WITO WA RAIS SAMIA KUANZISHA UFADHILI WA MASOMO

0
images (7)

Jumuiya ya Madola (Commonwealth) imeridhia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan wa kuanzisha mpango maalum wa ufadhili wa masomo wa Commonwealth Julius Nyerere Scholarship.

Mafanikio hayo yanatokana na majadiliano ambayo Mheshimiwa Rais Dkt.Samia aliyafanya na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo,Patricia Scotland katika Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar tarehe 04 Machi, 2024.

Aidha,uamuzi huo umefikiwa Ijumaa ya Machi 28,2025 ambapo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Patricia Scotland ametangaza rasmi kwamba jumuiya hiyo itaanzisha Scholarship Maalum itakayoitwa jina la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uingereza,Mbelwa Kairuki amesema, Scholarship hiyo itakuwa mahususi kwa ajili ya kufadhili masomo ya wanafunzi kutoka nchi za Afrika, Caribbean kusoma Shahada ya Uzamili (Masters) katika nchi zao.

“Hii ni mara ya kwanza Kiongozi wa Afrika anaenziwa na Jumuiya ya Madola kupitia jina la Scholarship.”

Balozi Kairuki amesema, mbali na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika jumuiya hiyo zipo pia Scholarship za Malikia Elizabeth.

Amebainisha kuwa, hii ni heshima kubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Na, ni matokeo ya kazi kubwa ya engagement ya Jumuiya ya Madola na Serikali yetu, itakumbukwa kuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan alikutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Zanzibar wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Jumuiya ya Madola na walizungumzia haja ya kuwezesha vijana kupata elimu na stadi za ufundi ili kuweza kufanya shughuli za kuwaletea kipato na kujikwamua kiuchumi.”

Lakini, pia Balozi Kairuki amebainisha kuwa, Mheshimiwa Patricia Scotland mara kadhaa amekuwa akielezea kufurahishwa kwake na hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali.

Ni katika kuboresha elimu kwa ajili ya vijana na kutoa fursa mbalimbali za elimu kwa vijana ikiwemo Samia Scholarship ambayo inatolewa kwa madaktari sambamba na Scholarship nyingine ambazo zimekuwa zikitolewa kwa Watanzania.

“Kwa hiyo, kutokana na kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais wetu, lakini kutokana na ushawishi wa Rais wetu kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.

“Pendekezo la kuanzisha Scholarship Maalum ijulikanayo kama Commonwealth Julius Nyerere Scholarship lililotoka kwetu Tanzania, limekubaliwa na Jumuiya ya Madola na sasa tutakwenda kushirikiana na Jumuiya ya Madola kwenye kuwezesha Scholarship hiyo kuanza kutumika kuanzia pengine mwaka ujao mara baada ya taratibu zote zikiwa zimekamilika, zimewekwa sawa.”

Balozi Kairuki amesema, kuna watu na taasisi mbalimbali ambazo zimepokea uamuzi huo kwa furaha na wako tayari kuchangia.

“Siku ya jana (Machi 28,2025) tu wakati wa uzinduzi taasisi moja ilionesha nia ya kuchangia takribani dola za kimarekani milioni 1 kwa kuanzia.

“Lakini, pia zipo taasisi nyingine ambazo Jumuiya ya Madola kwa kushirikiana nasi tutazungumza nazo ili ziweze kuchangia mfuko huu kwa kutoa udhamini kwa wanafunzi kutoka mataifa ya Afrika ambayo ni wanachama wa Jumuiya ya Madola na mataifa ya Caribbean.

“Kwa kweli hatua hii ni heshima kubwa kwa diplomasia yetu kwa sababu jina la Baba wa Taifa sasa linakwenda kuendelea kupaa katika Jumuiya ya Madola na mchango wake ndani ya Jumuiya ya Madola utaendelea kutambulika na kuenziwa kwa sababu historia yake itaendelea kuelezwa namna gani alichangia Jumuiya ya Madola kuanzisha Sekretarieti mpya hapa London.

“Na mabadiliko ya ajenda za Jumuiya ya Madola zijielekeze kwenye masuala ya msingi yanayogusa maisha ya wananchi hususani vijana, akina mama, walemavu na kadhalika.

“Kwa hiyo, hiyo ni heshima kubwa kwa nchi yetu na ni pongezi kubwa kwa Rais wetu na mwanadiplomasia namba moja kwa kuwezesha ili jambo na kwa kuchukua uongozi ameonesha njia na Jumuiya ya Madola imeitikia wito wake na ipo tayari kuanzisha hii programu.

“Kwa hiyo ni fursa pia kwa vijana wetu wengi ambao wanataka kusoma masomo ya elimu ya juu katika ngazi ya masters wataweza kusomea vyuo vikuu mbalimbali nchini na wataweza kupata ufadhili kusoma programu zao.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *