DAWASA YATOA MKONO WA EID KWA MAKUNDI YA WAHITAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika hatua ya kujali na kuthamini makundi maalumu katika jamii imetoa msaada wa mahitaji ya kibinadamu katika kituo cha Makao ya Kulea Watoto Yatima, kilichopo mtaa wa Nzasa, Kata ya Kijitonyama Wilaya ya Ubungo.
Hatua hii ni sehemu ya mpango wa Mamlaka wa kuthamini na kujali nafasi ya makundi maalumu katika jamii.

Akizungumza wakati wa utoaji wa msaada wa vitu mbalimbali vilivyowasilishwa ikiwemo vyakula, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa upo umuhimu mkubwa wa Jamii kuwajali na kuthamini makundi maalumu hususani watoto ambao wanaishi katika Mazingira magumu.
“Kwa kuwajali watoto hawa kutasaidia kuwatengeneza Mazingira mazuri katika ukuaji wao ili waweze kufanikiwa kiuchumi na kuweza kuwa viongozi wa baadae,” amesema Mhandisi Bwire.

Amepongeza kazi kubwa inayofanywa na walezi wa kituo hicho ya kuwatunza na kuwaongoza watoto hao katika misingi mizuri, na kuahidi DAWASA kuendelea kushirikiana na kituo hicho katika kusaidia ukuaji mzuri wa watoto hao ikiwemo kuchangia gharama za kuwasomesha shule pamoja na matibabu ya afya.
Kwa upande wake Hassan Hamisi mlezi Mkuu wa kituo hicho ameishukuru DAWASA kwa kuwajali na kuwashika mkono kwa mahitaji ya kibinadamu pamoja na kueleza nia ya Taasisi ya kuwasaidia kimasomo, “ni jambo la faraja sana kwetu kupata msaada wa kuendelea kuwalea watoto hao,” amesema.
Amesema kituo hicho kwa sasa kina jumla ya watoto 86 ambao wengine wanasoma na wengine bado ni wadogo wanaobaki kulelewa, hivyo misaada hiyo itatusaidia kuongeza ufanisi katika kuwahudumia na kuwakuza watoto hawa.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nzasa Ndugu Edwin Mfanga amesema kuwa kituo hiki kimekuwa sehemu ya mafanikio ya watoto wengi kwenye mtaa wa Nzasa.
Ameipongeza DAWASA kwa kuona haja ya kuwatembelea na kuwashika mkono, amewataka wanajamii wengine kuwakumbuka watoto hawa na kuwasaidia.