TMA,JNIA YATOA ELIMU KUSHEREHEKEA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI

0
IMG-20250323-WA0002

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kupitia Kituo cha Hali ya Hewa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), imeadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa kutoa elimu kwa wadau pamoja na kuweka mipango ya kuendelea kuboresha huduma na kuongeza tija na ufanisi katika kuhakikisha usalama wa usafiri wa anga.

Akizungumza leo Machi 23, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi waliotembelea kituo cha hali ya hewa cha JNIA, Meneja wa TMA Huduma za Hali ya Hewa Usafiri wa Anga na Msimamizi wa Kituo cha Hali ya Hewa JNIA, Bw. John Mayunga, amesema kuwa ni muhimu kuelimisha jamii ili waweze kuchukua tahadhari na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Bw. Mayunga ameongeza kuwa, kuna mchango mkubwa katika utoaji wa tahadhari kabla ya jamii kujikuta katika athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kwani majanga mengi duniani yamehusishwa na hali mbaya ya hali ya hewa.

“Tumeboresha mifumo ya kutuma taarifa za hali ya hewa ili kuwafikia wateja wetu kwa wakati, kwa sasa tunatumia teknolojia ya kisasa yenye uwezo wa kujiendesha yenyewe,” amesema Bw. Mayunga.

Aidha, ameeleza kuwa maadhimisho haya ni sehemu ya kufanya tathmini ya kitaalamu kuhusu utoaji wa huduma na kutoa elimu kwa wadau juu ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

Msimamizi wa Kituo cha Uangazi TMA – JNIA, Bw. Ally Selemani, amesema kuwa wanajivunia kutumia teknolojia ya kisasa ambayo imewawezesha kutoa taarifa za uhakika za hali ya hewa pamoja na kupunguza changamoto kwa asilimia kubwa katika utendaji wa kazi.

“Kadri siku zinavyozidi kwenda, tunaendelea kufanya maboresho ya vifaa vyetu vya kukusanya data kwa ajili ya kuandaa taarifa mbalimbali za hali ya hewa. Tumepiga hatua kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma,” amesema Bw. Selemani.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi, Ivan Yona na Jackline Raphael kutoka Shule ya Msingi Michael Mausa, wameishukuru TMA kwa kuwaelimisha kuhusu utendaji wa kazi zao, jambo ambalo linawasaidia kuwa na uelewa zaidi kuhusu matumizi ya taarifa za hali ya hewa na jinsi ya kukabiliana na athari zinazoweza kutokea.

Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani 2025 yamebeba kauli mbiu isemayo “Kwa Pamoja Tushughulikie Pengo la Utoaji wa Tahadhari”.

imeandaliwa na Noel Rukanuga – DSM.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *