MCHENGERWA ASHUHUDIA UTIAJI SAINI WA MIKATABA YA UJENZI WA BARABARA KM. 84 ZA DAR ES SALAAM

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Machi 21, 2025 ameshuhudia Utiaji Saini wa Zabuni 9 zilizobeba thamani ya Shilingi Bilioni 221.8 zinazojumuisha Barabara zenye urefu wa Kilomita 84.4 zinazotarajiwa kujengwa katika Halmashauri za Dar es Salaam chini ya Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II).
Miongoni mwa zabuni Hizo, Zabuni 2 zenye Jumla ya thamani ya Sh.Bil 47.1 ni kwa ajili ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ambapo Bilioni 25.9 zitakwenda kutengeneza Barabara za Masuliza, Kilimahewa na Tuangoma zenye jumla ya kilomita 10.21 huku Bilioni 21.1 zikielekezwa kwa ajili ya Barabara za Konisaga 1, Konisaga 3, Kurasini, Taningira uhasibu, Kizota, Lushoto, Pendamoyo, Mandera, Mkumba Miburani, Kipati pamoja na Vivuko 6 vya Mdeda, Mpeta, Baajun, Msalaka Mashine ya maji, Shehe muckhi, na Azimio Msalaka.


Akizungumza katika Hafla hiyo Mhe. Mchengerwa amesema Matarajio ya Rais wetu ni kulifanya Jiji la Dsm kuwa Miongoni mwa Majiji ya Kisasa, Jiji shindani (Metropolitan city) na fedha hizi ni za Watanzania, Wakandarasi wanapokabidhiwa Mikataba hii waende kuitendea haki, na Wakandarasi walioshindwa kutimiza Makubaliano naelekeza kutengua Mikataba, taratibu zote zifuatwe bila kuingiza hasara Serikali maana yake ni lazima walipe fedha zote walizopewa na Serikali. Taratibu hizi zianze na ntaanza kuzifatilia kwa katibu mkuu”
“Na Kampuni hizi tulizozipa Kazi leo hii kusaini Mikataba wasipotekeleza makubaliano na kushindwa kutekeleza kwa muda tuliokubaliana taratibu za kuvunja Mkataba zifuatwe na wawe blacklisted wasiruhusiwe kupata Mkataba wowote ndani ya Nchi hii. Kwenye Mikataba hii tuliyosaini leo hatutakuwa na nyongeza hata siku moja”. Alisema Mhe. Mchengerwa.
Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Mradi (Millenium Tower) na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali.