SERIKALI KUTUMIA 174.36 MILIONI KUANZISHA MRADI WA MAZIWA KATIKA MIKOA 10


Dodoma.Katika kuendeleza na kufanya juhudi za kuimarisha na kuweka mikakati bora ya kukuza tasnia ya Maziwa nchini serikali imetambulisha Mradi mpya wenye thamani ya Dola Sh 174.36 milioni za Kimarekani.
Hayo yameelezwa leo Machi 18, 2025 mkoani Dodoma, na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe, katika Warsha hiyo ya kutambulisha Mradi huo wa Kimageuzi wa Tasnia ya Maziwa.
Shemdoe amesema kuwa mradi huo uzingatie thamani ya fedha, muda pamoja na matokeo chanya yanayolenga kuwanufaisha vijana, wakina mama pamoja na makundi maalum
“tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kuwepo kwa Mradi huu” amesema Shemdoe
Aidha Shemdoe ameeleza kuwa Mradi huo ni Muunganiko wa upande wa Tanzania Bara na Visiwani unaotarajiwa kufika katika Mikoa 10 na Wilaya 28.

Amewashukuru wadau wa maendeleo pamoja na wadhamini ambao ni IFAD, OPEC Fund, AFD, Irish League of Credit Union’s Foundation (ILCUF), HEIFER, International Tanzania (HI), Tanzania Agricultural Development Bank (TADB) na FAO.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo – Zanzibar, Ali Khamis Juma, amesema Mradi huo unategemewa kuinua kipato na maisha ya Mtanzania hususani kwa wafugaji kwani Serikali imejipanga kushirikiana na wafugaji wadogo na kuwasaidia kukua katika tasnia ya Maziwa.
“Tunaamini kwamba tukiweza kukamilisha mradi huu kikamilifu baada ya miaka kumi tunaenda kushuhudia maendeleo makubwa kwa wananchi wetu”
Juma amesema kuwa shauku yake ni kuona makundi mbalimbali hasa ya vijana yakichangamkia fulsa kwenye mradi huo
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael, amesema Maziwa yanachangia kwa asilimia 30% ya pato la Taifa, japo kunahitajika kuhakikisha upatikanaji wa Maziwa unatakiwa kuwekewa Mazingira mazuri ikiwemo kuboresha Malisho na upatikanaji wa maji, Huduma za Ugani, Tafiti, mafunzo na Masoko kwa ajili ya wafugaji.