BODI YA USHAURI YA TARURA YAKAGUA MAENDELEO YA MIRADI ILIYOJENGWA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA MBADALA

0

Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi iliyojengwa kwa kutumia teknolojia mbadala jijini Dodoma.

Miradi hiyo ni ujenzi wa barabara Km.  6.95 kwa kutumia teknolojia ya ‘Ecoroads’ iliyopo wilayani Chamwino pamoja na ujenzi wa daraja la mawe la Nghong’ona lenye urefu wa mita 26.44 na upana wa mita 7 lililopo kata ya  Nghong’ona jijini  Dodoma.

Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Mwenyekiti wa Bodi Mhandisi Florian Kabaka amesema kuwa, lengo la kukagua miradi hiyo ni kuona utendaji wa teknolojia mbadala ili kuona kama inafaa kutumika katika maeneo mengine nchini.

“Teknolojia hii ni mpya kwetu hivyo ni muhimu tuangalie na kukagua mara kwa mara kuona kama zinatufaa ama la, kwa upande wa teknolojia ya ‘Ecoroads’ ndio tumeanza kuitumia na barabara ina miezi 7, kwa mazingira na udongo wa nchi yetu bado tunahitaji kujifunza zaidi tuone kama inafaa kwetu”, amesema.

Kuhusu ubora wa madaraja ya mawe, Mhandisi Kabaka ameeleza kuwa yanafanya vizuri na yanatumia gharama ndogo, ukilinganisha na madaraja ya zege na nondo ambapo na hivyo amewataka TARURA kufanya usimamizi na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa miundombinu hiyo.

Aidha, Mhandisi Kabaka ametoa wito kwa wananchi kuilinda miundombinu iliyopo kwenye maeneo yao ili iweze kudumu kwa muda mrefu, aidha, amewataka wananchi watoe taarifa mapema kama kukitokea uharibifu wa miundombinu katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA mkoa wa Dodoma, Mhandisi Edward Lemelo amesema teknolojia ya ‘Ecoroads’ ni kemikali zinazochanganywa kwenye udongo ili kupunguza gharama katika ujenzi wa barabara ambapo wanaendelea kufanya ufuatiliaji ili kuona ubora wa teknolojia hiyo kwa lengo la kutumia katika kazi zao kwa ujumla.

Ameongeza kuwa madaraja ya mawe wameona yanapunguza gharama na mpaka sasa katika mkoa wa Dodoma wamejenga madaraja 9 huku madaraja 8 ujenzi wake ukiwa unaendelea na mpango kwa mwaka ujao wa fedha ni kujenga madaraja makubwa 2 ambapo kwa kipindi kifupi watakuwa wamejenga madaraja 19 ya mawe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *