SERIKALI YAENDELEA KUSISITIZA MATUMIZI YA ADHABU MBADALA

0

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa matumizi ya adhabu mbadala kwa wahalifu wa makosa madogo badala ya vifungo Magerezani, ikiwa ni hatua muhimu ya kupunguza msongamano wa wafungwa na kuimarisha mifumo ya haki jinai nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Jamii jijini Dodoma leo Machi 10, 2025.

Naibu Waziri Sillo amesema adhabu mbadala siyo tu inapunguza gharama za kuhudumia Wafungwa, bali pia inawapa fursa Wahalifu wa makosa madogo kujirekebisha huku wakiendelea kuchangia maendeleo ya jamii.

“Serikali yetu inaendelea kusisitiza matumizi ya adhabu mbadala kama njia ya kuhakikisha haki inatendeka bila kuongeza mzigo kwa Magereza yetu. Adhabu hizi zinawasaidia Wahalifu wa makosa madogo kubadilika huku wakiendelea na maisha yao ya kawaida badala ya kukaa Gerezani,” Amesema Sillo.

Aidha, aliitaka Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Jamii kusimamia kwa dhati utekelezaji wa Sheria ya Huduma kwa Jamii Sura ya 291, pamoja na kuelimisha Wananchi kuhusu faida za adhabu mbadala. Alibainisha kuwa bado kuna changamoto ya mtazamo wa jamii, ambapo wengi wanaamini kuwa adhabu pekee kwa Mhalifu ni kifungo Gerezani.

Mhe. Sillo pia alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha Taasisi za Haki Jinai kwa kuziongezea bajeti na rasilimali ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Vilevile Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Jamii, Jaji Stephen Magoiga, amesema uelewa wa jamii kuhusu adhabu mbadala bado ni mdogo licha ya utekelezaji wake kuendelea. Amesisitiza kuwa Kamati yake itaweka mkazo katika kutoa Elimu ili mfumo huu utambulike na kukubalika zaidi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uangalizi, Charles Nsanze amesema Serikali imefanikiwa kupunguza msongamano Magerezani kwa kuwezesha Wafungwa 8,170 kutumikia adhabu zao nje ya Magereza kati ya Julai 2022 na 2024 ambapo mpango huo umesaidia kuokoa Shilingi Bilioni 29 na Milioni 412 ambazo zingetumika kwa chakula, huku Wafungwa wakichangia maendeleo kupitia kazi za kijamii kama ujenzi wa Shule, utunzaji wa Mazingira na Uchimbaji wa vyoo vya Umma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *