WANAWAKE WA NHC WASHEREKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

0

Wafanyakazi wanawake wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wameungana na wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika leo Machi 8, 2025, katika Viwanja vya Leaders Club. Huku Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila ametoa pongezi kwa wanawake kwa mchango wao mkubwa katika Taifa kupitia shughuli wanazozifanya katika taasisi za umma na sekta binafsi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Chalamila amesema kuwa mwanamke ni dira, mjenzi, mbunifu, hivyo wakipewa nafasi katika jamii, watafanya kazi kwa ufanisi na kuleta maendeleo kwa Taifa.

RC Chalamila amesisitiza umuhimu wa wanawake kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kuungana kupiga mfumo kandamizi ambao unakwamisha maendeleo katika nyanja mbalimbali.

“Serikali itaendelea kupinga unyanyasaji wa ukatili wa kijinsia pamoja na mfumo dume ambao umekuwa sio rafiki katika jamii, kwani kuna baadhi ya watu bado wanafanya matendo ya ukatili,” amesema Mhe. Chalamila.

Afisa Tawala Mwandamizi wa NHC, Limi Mihama, amesema kuwa Shirika la Nyumba la Taifa linatambua mchango wa wanawake na kutoa fursa ya kushiriki katika maadhimisho hayo, kwani mwanamke ni msingi wa nyumba kutokana na uwezo wao wa kusimamia shughuli mbalimbali na kuleta matokeo chanya.

Mihama ameongeza kuwa wanawake ni jeshi kubwa, hivyo ni fursa kwao kuungana na wanawake wote duniani kuadhimisha siku hiyo muhimu, huku akitaja mfano wa wahandisi wanawake wanaofanya vizuri katika kusimamia miradi mbalimbali NHC ikiwemo Mradi wa Samia Scheme, unaotekelezwa katika eneo la Kawe, Dar es Salaam.

Afisa Utumishi Mwandamizi wa NHC, Lilian Mushi, amesema kuwa wanajivunia utamaduni wa Shirika kutoa kipaumbele kwa wanawake katika kusimamia idara mbalimbali na miradi mikubwa pamoja na kuendelea kutekeleza mipango ya kuhakikisha kila mtanzania anapata makazi bora kwa gharama nafuu.

“Wanawake tunajivunia maadhimisho ya mwaka huu, kwani Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ushirikiano mkubwa ikiwemo kutoa mikopo ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wanawake kuendesha maisha yao,” alisema Mushi.

Maadhimisho haya ya Siku ya Wanawake Duniani, yamebeba kauli kauli mbiu : “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” ambapo yamekuwa ya kipekee, kwani wameonesha umoja wa wanawake katika harakati za maendeleo na usawa katika jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *