WATENDAJI WA UBORESHAJI WA DAFTARI WAASWA KUWAHAMASISHA WANANCHI

0

Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari kutoka halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam leo Machi 07,2025.


Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari kutoka halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam leo Machi 07,2025.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akifafanua jambo. 

Washiriki wa Mafunzo hayo wakifuatilia Hotuba ya kufunga mafunzo hayoNa. Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwahamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao.
 
Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari kutoka halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam.
 
Mafunzo hayo ya nadharia na vitendo namna ya kutumia vifaa vitakavyotumika kwenye zoezi hilo ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa daftari mkoani humo ambao utaanza tarehe 17 hadi 23 Machi, 2025.
 
“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao,” amesema Jaji Mbarouk. 
 
Ameongeza kuwa Tume inatarajia kuwa baada ya zoezi hilo kukamilika watu watakaokuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura halali.
 
“Jukumu la uhamasishaji linawahusu moja kwa moja ninyi watendaji, kwa kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yenu kupitia nyenzo mlizo nazo,” amesema Jaji Mbarouk.
 
Amewasisitiza kuhakikisha kuwa sambamba na kuwahamasisha wananchi wasambaze mabango waliyopewa na Tume kwenye maeneo yao ya kiutendaji ili wananachi wapate habari za kina kuhusu zoezi hilo.
 
“Mabango na vipeperushi mtakavyopewa na Tume mvisambaze mapema katika kata zote zilizopo katika halmashauri zenu na kutokea huko yafike vituoni ili iwe rahisi kwa wapiga kura na wadau wengine kujua vituo viko wapi,” amesema.
Jaji Mbarouk amewaasa kuwa licha ya shughuli nyingi za kiutendaji walizonazo watendaji hao wafuatilie kwa karibu zoezi hilo na kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha kuwa linafanikiwa.
 
Kuhusu watumishi wa vituoni, Jaji Mbarouk amesema “ni vyema kuwasisitiza watendaji walio chini yenu kuzingatia matumizi ya lugha nzuri pamoja na kufanya kazi vituoni muda wote hata kama hakuna waombaji wanajitokeza.”.
 
 
Katika hatua nyingine Jaji Mbarouk amewakumbusha watedaji hao kuhusu uwepo wa mawakala wa vyama vya siasa na kuwasisitiza kuhusu umuhimu wa kuwapa ushirikiano kwa kuwa ni wadau muhimu.
 
“Wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura hivyo wapewe ushirikiano,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *