WAKAZI WA DAR, PWANI NA MOROGORO KUPATA MAJI YA UHAKIKA

0

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amesema kukamilika kwa Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda kutahakikisha upatikanaji wa huduma ya uhakika ya majisafi kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, baadhi ya maneo ya Mkoa wa Morogoro na Pwani kutokana na upatikanaji wa maji kwa muda wote katika Mto Ruvu.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda, wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 335 ambazo ni fedha za ndani za Serikali na kutaka utekelezaji wa mradi.

Katika hotuba yake, Mhe. Majaliwa amesema kuwa bwawa hilo ni mradi wa kimkakati wenye lengo la kuhakikisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa Jiji la Dar es Salaam, pamoja na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Morogoro na Pwani. Amesema kuwa mradi huo ili uweze kufanikiwa kutimiza lengo lake ni lazima vyanzo vya maji vitunzwe ili bwawa liweze kujaa.

Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji kitaifa katika ngazi zote za mikoa. Amesema kuwa ajenda ya utunzanji wa mazingira na vyanzo vya maji ni ya kudumu kwa kila Mtanzania.

“Fedha za utekelezaji wa miradi ya maji zipo, ila uharibifu wa vyanzo vya maji ni changamoto kubwa katika adhma ya Serikali kufikisha huduma ya maji kwa wananchi. Hivyo, hatuna budi kulinda na kutunza vyanzo vya maji.” Waziri Mkuu ametoa rai.

“Nawaagiza Wakurugenzi wote wa Mabonde ya Maji nchini msikae ofisini, wekeni mipango ya kutembelea mabonde mnayosimamia na kuyajua vizuri. Hakikisheni matumizi mazuri ya maji yanazingatiwa kwa kufuata taratibu na sheria; mnatoa elimu ya kulinda na kutunza vyanzo vya maji pamoja na kutoa hamasa na motisha kwa wananchi wote wanaotunza vyanzo vya maji katika maeneo yao” Mhe. Majaliwa ameelekeza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amezindua rasmi Wiki ya Maji Kitaifa mwaka 2025 kuanzia leo yenye Kaulimbiu “Utunzaji wa Uoto wa Asili kwa Uhakika wa Maji’ sanjari na uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi wa miradi ya maji na shughuli za kijamii katika maeneo mbalimbali nchini.

Naye, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema mradi huo unagharamiwa kwa fedha za ndani za Serikali, ambapo mpaka sasa mkandarasi anayetekeleza mradi huo Sinohydro Corporation Ltd kutoka China ameshalipwa Sh. Bilioni 85 kwa awamu ya kwanza na mradi umefikia asilimia 28 ya ujenzi na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Novemba, 2026.

Ujenzi wa Bwawa la Kidunda ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, inayolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata majisafi, salama, na ya kutosha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *