MAPAMBANO UPOTEVU WA MAJI DAR, WENYEVITI WA MITAA KUPEWA ‘VOCHA’

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika lengo la kuimarisha ushirikiano baina na Viongozi wa Serikali za Mitaa, imeanzisha motisha maalum ya kuwawezesha Viongozi hao kuwa sehemu ya kundi muhimu la kuzuia upotevu wa maji mitaani.
Akizungumza na Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Ubungo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa, hatua ya kuwashirikisha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ni kwa lengo la kuboresha huduma za Maji na kila mwananchi kupata taarifa sahihi na za wakati kuhusu huduma hii ya majisafi.

Ameongeza kuwa katika kufanikisha hili, Mamlaka imeandaa motisha maalumu ya muda wa maongezi kwa Wenyeviti wote wa Serikali za Mitaa katika Mkoa wa Dar es salaam ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa kukusanya taarifa muhimu zinazohusu huduma ya majisafi na usafi wa mazingira na kuzitoa kwa DAWASA ili hatua ya maboresho ziweze kuchukuliwa na kufanyiwa kazi.
“Tumeona tuwawezeshe Wenyeviti hawa kwa kuwapa vocha kiasi kidogo kila mmoja kwa kila Mwezi ili waweze kufanya kazi hii kwa ufanisi zaidi,” amesema Mhandisi Bwire
Sambamba na hilo, Mhandisi Bwire amesema kuwa Mamlaka inakusudia kutoa zawadi maalum kwa Wenyeviti wa mitaa watakapofanikiwa kuwahamasisha wananchi kulipa madeni yao ya maji na waliositishiwa huduma kufunguliwa huduma ili kuendelea kutumia maji ya DAWASA.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Ukombozi , ndugu Innocent Mazigo amesema kuwa hatua ya DAWASA kuamua kushirikisha viongozi hao kwenye utoaji wa huduma ni hatua mzuri sana kwa kuwa inaonesha kuthamini nafasi yetu na kazi yetu kwa wananchi.
“Sisi tuko tayari kushirikiana na Taasisi za mfano kama DAWASA kwa kuwa huduma ya majisafi ni huduma muhimu kuliko zote na zisizokuwa na mbadala wake,” amesisitiza ndugu Mazigo