TANZANIA NI SALAMA KWA UWEKEZAJI, SERA ZA UWEKEZAJI NI RAFIKI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumamosi Machi Mosi, 2025 ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kituo cha gesi cha GBP mkoani Tanga, mradi unaogharimu dola milioni 50.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesema kuwa mradi huo ni muhimu kwa maendeleo ya Tanga na Taifa kwa ujumla, kwani utaunga mkono ajenda ya nishati safi ya kupikia na pia kuchochea ukuaji wa viwanda mkoani Tanga.
“Uwekezaji huu (wa ujenzi wa kituo cha gesi cha GBP Tanga) ni mkubwa, na utachochea matumizi ya nishati safi ya kupikia na pia utasaidia katika sekta ya viwanda, ambavyo tumedhamiria vifunguliwe kwa wingi hapa Tanga,” alisema Rais Samia.
Rais Samia ameeleza pia kuridhishwa na hatua ya GBP katika kusambaza mafuta kwa ukanda wa Kaskazini na akashauri Serikali kupitia Wizara ya Nishati kutekeleza sera zinazowezesha maeneo ya Tanga kuwa kituo kikuu cha kusambazia mafuta kwa ukanda huo.
Pia, Dkt. Samia ameongeza kwa kusema kuwa, GBP ina mipango ya kuwekeza katika sekta mbalimbali kama vile kujenga kisima cha kuhifadhi mafuta, kiwanda cha vilainishi, na kuwekeza zaidi katika visima vya Unguja na Pemba.
Amesisitiza kuwa, serikali itaendelea kuunga mkono uwekezaji huo mkubwa na kuhakikisha kuwa sera za biashara na uwekezaji zinahamasisha ukuaji wa uchumi na ustawi wa Taifa.
“Tunataka kuhakikisha kuwa kila mkoa unapata vituo vya kujaza gesi. Huu ni uwekezaji mkubwa na Serikali inawaahidi wawekezaji kuwa itawapa ushirikiano mkubwa katika jitihada zao,” alisisitiza Rais Samia.
Katika hotuba yake, Rais Samia pia alisisitiza umuhimu wa mradi huu kwa wananchi wa Tanga, akisema kuwa unatarajiwa kutoa ajira 1,000 na kuchochea mzunguko wa fedha katika mkoa huo.
Ameahidi kuwa mradi huo utamalizika kwa wakati na kuleta manufaa kwa wananchi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla.
“Nina imani kuwa mradi huu utamalizika mapema na wananchi wa Tanga watafaidika na ajira na mzunguko wa fedha,” alisema.
Rais Samia ameongeza kuwa, Tanzania imefunguka kwa uwekezaji na kuwa ni salama kwa wawekezaji, huku sera za uwekezaji zikiwa rafiki na endelevu.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania itahakikisha kuwa mazingira ya uwekezaji yanabaki kuwa ya kuvutia, ikiwa ni pamoja na kuwa na sera zinazowawezesha wawekezaji kuwa shindani katika soko la ndani na kimataifa.
“Niwahakikishie GBP na wawekezaji wengine kuwa Tanzania ni salama kwa uwekezaji na sera zetu za biashara ni rafiki na endelevu,” alihitimisha Rais Samia.