MWANANCHI KUPATA KITAMBULISHO CHA NIDA NDANI YA SIKU 14 – BASHUNGWA

0

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameeleza mkakati wa Serikali ni kuhakikisha Mwananchi anapata Kitambulisho cha Taifa ndani ya siku 14 mara baada ya kukamilisha usajili katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Ameeleza hayo, tarehe 28 Februari 2025 katika hafla ya Jubilei ya miaka 25 ya huduma ya Kolping Hotel, Bukoba Kagera ambapo alitumia nafasi hiyo kueleza mikakati ya Serikali katika kuboresha utoaji wa huduma za NIDA kwa wananchi.

“Mkakati uliokuwepo kwa sasa, mwananchi atakapojisajili ndani ya siku 7 atapokea namba yake ya NIDA (NIN) katika namba ya simu aliyoijaza kwenye fomu na baada ya siku 14, atapokea ujumbe mwingine wa kumtaarifu kufuata kitambulisho chake katika ofisi za NIDA” amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa amewaagiza viongozi wa NIDA ngazi za Wilaya na Mikoa kutoa elimu kwa Wananchi juu ya mpango mpya wa utoaji huduma ambao umelenga kuondoa kero zote zilizokuwa zinalalamikiwa na wananchi kuhusu usajili, uzalilshaji na
usambazaji wa vitambulisho hivyo.

Aidha, Bashungwa ameielekeza NIDA na Idara ya Uhamiaji kukaa pamoja katika kila ofisi za wilaya, ili kuhakikisha huduma za usajili na utambuzi zinawafikia
wananchi bila usumbufu.

Ametoa rai kwa wananchi wenye changamoto ya kukosa namba na kitambulisho, kujitokeza wakati NIDA na Idara ya Uhamiaji wanapofanya zoezi la uhakiki au usajili katika maeneo yao ili kupata huduma na kutatua changamoto hizo.

Katika Mkoa Kagera, Bashungwa amemuagia Afisa Msajili NIDA kuweka kambi wilaya zote ili kuwasajili wananchi ambao wametimiza miaka 18, ambapo zoezi hilo litaanza tarehe 10 Machi 2025 katika Wilaya ya Kyerwa.

Bashungwa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwasajili wananchi 269,177 katika Mkoa wa Kagera ambao wametimiza miaka 18 ambao awali waliokosa nafasi ya kujisajili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *