BAADA YA MABORESHO MAKUBWA BANDARI YA TANGA, SHEHENA YAONGEZEKA MARA NNE, MELI ZAIDI YA 300 ZAPOKELEWA KWA MWAKA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kusimamia maboresho makubwa katika sekta ya uchukuzi, hususan katika Bandari ya Tanga, ambayo sasa ina uwezo wa kuhudumia meli kubwa moja kwa moja kutoka nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Machi Mosi, 2025 na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na kubainisha kuwa, serikali imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 419.16 katika maboresho ya Bandari ya Tanga, jambo ambalo limeleta matokeo makubwa, ikiwemo ongezeko la shehena kutoka tani 750,000 hadi tani 3,000,000 kwa mwaka.
“Pia, idadi ya meli zinazoingia bandarini imeongezeka kutoka meli 118 mwaka 2019/2020 hadi kufikia meli 307 mwaka 2023/2024.” alisema Profesa Mbarawa.


Katika hatua nyingine, maboresho haya yamesababisha kupungua kwa muda wa kuhudumiwa kwa meli kutoka siku tano hadi siku mbili, jambo lililopunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ushindani wa bandari hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Zaidi ya hayo, mapato ya Bandari ya Tanga yameongezeka kwa kasi kubwa, ambapo ndani ya miezi saba tu ya mwaka wa fedha 2024/2025, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekusanya shilingi bilioni 49.84.
Maboresho haya pia yamechangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la ajira, ambapo kabla ya maboresho, bandari ilikuwa ikiajiri wastani wa wafanyakazi wa muda mfupi 6,630 kwa mwezi, lakini sasa imefikia wastani wa 17,871 kwa mwezi.
Ameongeza kwa kusema kuwa, Serikali imeendelea kusimamia maendeleo zaidi katika sekta ya uchukuzi mkoani Tanga, ambapo miradi mbalimbali yenye thamani ya shilingi trilioni 1.1 inatarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Miradi hiyo inahusisha ukarabati wa reli inayoingia bandarini yenye urefu wa kilometa 3.9 pamoja na kituo cha reli ndani ya Bandari ya Tanga, mradi unaotarajiwa kugharimu shilingi milioni 980.
Ukarabati wa reli kutoka Ruvu hadi Tanga yenye kilometa 248 na ile ya Mruwasi hadi Arusha yenye kilometa 414 pia ni sehemu ya miradi hiyo, ambapo mikataba yenye thamani ya dola milioni 132 (takriban shilingi bilioni 329) imesainiwa.
Ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 kwa ajili ya kuhudumia makasha unatarajiwa kuanza Agosti mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 480.
Aidha, serikali imepanga kujenga gati jipya la kupokelea mafuta katika eneo la Raskazone kwa gharama ya shilingi bilioni 180 ili kuongeza ufanisi wa bandari hiyo.
Katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga, Waziri Mbarawa amesema, serikali inatarajia kufanya ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Tanga, mradi unaojumuisha ujenzi wa njia ya kurukia na kutua ndege, maegesho ya ndege, njia za maungio, pamoja na ujenzi wa jengo la abiria na uwekaji wa taa za kuongozea ndege.
Ukarabati huo utagharimu shilingi bilioni 91.89 na mkataba wa mradi huu unatarajiwa kusainiwa Machi 2025.
Katika kuhakikisha usalama wa baharini unaimarishwa, serikali itanunua boti mpya za doria, ufuatiliaji na uokoaji zenye kasi ya knots 40, ambazo pia zitasaidia shughuli za ukaguzi wa vyombo vya baharini. Boti hizi za kisasa zitagharimu shilingi bilioni 2.62 na mkandarasi wa mradi huu tayari amepatikana.
Ili kuhakikisha usafiri wa mizigo unakuwa wa haraka, serikali inapanga kujenga barabara mpya ya Handeni-Kiberashi-Kijigu-Mrijo-Dalai-Chemba-Kwa Mtoro-Singida yenye urefu wa kilometa 340 kwa gharama ya shilingi bilioni 432.5.
Barabara hiyo ikijengwa, itaweza kupunguza umbali wa safari kwa takribani kilometa 250, hivyo kupunguza matumizi ya mafuta kwa lita 100-120 kwa safari moja.Serikali inapanga kutumia mfumo wa PPP (Public-Private Partnership) ili kuhakikisha barabara hii inakamilika kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Wizara ya Uchukuzi kupitia TPA ipo katika mazungumzo na Wizara ya Kilimo ili kuhakikisha pembejeo zote za kilimo zinaingizwa nchini kupitia Bandari ya Tanga lengo ni kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuimarisha nafasi ya Bandari ya Tanga kama kitovu cha biashara.
Pia, TPA itaweka eneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa gati kwa mwekezaji wa kiwanda cha sukari, hatua itakayopunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa hizo ndani na nje ya nchi.
Kutokana na maboresho hayo makubwa, Bandari ya Tanga sasa ni kivutio kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, hususan kutoka Uganda, Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Waziri huyo wa Uchukuzi amesema kuwa, serikali itaendelea kuwekeza ili kuhakikisha Tanga inarudi katika hadhi yake kama mji wa viwanda, biashara, na uchukuzi wa kimataifa.
Miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha uchumi wa Afrika Mashariki kwa kuboresha sekta ya uchukuzi na miundombinu ya usafirishaji.