ZINGATIENI THAMANI YA FEDHA KATIKA UJENZI WA MIRADI YA AFYA – DKT. MFAUME

Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume, amewataka wasimamizi na watumishi kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa sekta ya afya ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora.
Dkt. Mfaume ametoa kauli hiyo alipotembelea Kituo cha Afya cha Serya, kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa, ambapo ameanza ziara yake ya kukagua huduma za afya, lishe, na ustawi wa jamii katika Mkoa wa Dodoma.


Amesema kuwa serikali imekuwa ikitafuta fedha mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya ili kuboresha huduma kwa wananchi, hivyo ni muhimu kwa wasimamizi na watendaji kuzingatia ubora na ufanisi katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, Dkt. Mfaume ameendelea kuhamasisha matumizi ya mapato ya ndani katika ujenzi na ukamilishaji wa miradi ya afya.
“Tumeona hapa Zahanati ya Ausia imejengwa kwa mapato ya ndani kwa asilimia 100, hivyo nitoe rai kwa halmashauri zenye mapato makubwa kutenga sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya afya,” amesema Dkt. Mfaume.


Ameongeza kuwa kuna maboma mengi yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi, na halmashauri zenye mapato makubwa zinaweza kutenga fedha kidogo ili kukamilisha ujenzi huo, hivyo kuharakisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa jamii.