RAIS SAMIA AWATAKA MAAFISA MASUULI KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO IKAMILIKE KWA WAKATI

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Mkoani Tanga kuzungumza na wananchi wa Tanga Mjini kwenye viwanja vya Mkwakwani, amewataka Maafisa masuuli wanaosimamia miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani Tanga kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha miradi yote ya maendeleo mkoani humo inakamilika kwa wakati.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Februari 28, 2025 wakati akizungumzia changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa ziara yake ya siku tano kwenye Wilaya zote za Mkoa huo akisema ipo changamoto ya kusuasua kwa miradi ya maendeleo suala ambalo linachelewesha maendeleo kwa baadhi ya maeneo.

Rais Samia pia amesema amelichukua ombi la wananchi wa Tanga pamoja na viongozi wao mbalimbali kutaka chuo kikuu kujengwa Mkoani humo, akisema serikali tayari imeanza kulifanyia kazi suala hilo kwa kuanzisha kampasi ya Chuo kikuu cha Mzumbe kwenye Mji wa Mkinga na kumuagiza Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda kufanyia kazi ombi la ujenzi wa chuo kikuu mkoani humo.

Rais Samia ametumia Mkutano huo pia wakati huu Waumini wa dini ya Kiislamu wakisubiri mwandamo wa mwezi kuwatakia Funga njema na yenye kheri waislamu wote nchini sambamba na Kuwatakia waumini wa dini ya Kikristo kuwa na mfungo mwema wa kwaresma, wakati huu wakijiandaa na Mfungo huo kuelekea sikukuu za Pasaka kwa mwaka 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *