SERIKALI KUENDELEA KUWEZESHA USHIRIKI WA SEKTA BINAFSI KATIKA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kutunga Sera
rafiki zitakazowezesha ushiriki wa sekta binafsi katika upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa bei nafuu.

Ameyasema hayo leo Februari 27, 2025 akiwa wilayani Muheza katika muendelezo wa ziara yake mkoani Tanga ambapo amezindua zoezi la ugawaji wa mitungi ya gesi ya kupikia kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga.

“Tumeanza kutoa ruzuku kwa wale wote wenye miradi ya gesi ambao wanachakata na kuifanya gesi kuwa nishati”. Amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa, Serikali pia inatoa ruzuku hadi kwenye majiko ya umeme ili kuwezesha watanzania wengi zaidi kutumia nishati safi ya kupikia.

Amepongeza ubunifu wa teknolojia mbalimbali ambazo zinakwenda kubana matumizi katika kutumia nishati safi ya kupikia.

Amesema lengo la Serikali ni kulinda afya za watumiaji wa Nishati za kupikia pamoja na mazingira.

Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara ya Nishati kuendelea kuusimamia mkakati wa nishati safi ya kupikia ili kuweza kufikia lengo la asilimia 80 ya watanzania kutumia nishati safi ya kupikia kufikia mwaka 2034.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema upatikanaji wa umeme maeneo ya vijijini uwe zaidi ya kuwasha taa na kuchaji simu bali utumike pia katika shughuli za kiuchumi.

Awali Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga alimpongeza Rais Samia.kwa kukubali kuzindua programu ya ugawaji mitungi ya gesi ya ruzuku 452,445.

Mhe. Kapinga alisema mpango.huo jumuishi utasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira na kupunguza athari za kijamii kiafya na kiuchumi.

“Mhe. Rais programu yako hii imezaa matunda, tunapoelekea mwaka mmoja wa utekelezaji wa mkakati huu wa nishati safi ya kupikia kama Taifa tumepiga hatua sana”. Amesema Mhe. Kapinga

Ameeleza kuwa, kupitia sekta binafsi usambazaji gesi kabla ya Mkakati ulikuwa ni asilimia kumi hadi 11 kwa mwaka ila kwa sasa ukuaji wa kampuni hizo ni asilimia 50 hadi 60 kwa mwaka.

Aliongeza kuwa kiashiria Kingine cha ukuaji wa matumizi ya nishati safi ni ongezeko la masoko vijijini lakini hamasa kubwa ya nishati safi ya kupikia imekuja pia kutokana na uwepo wa umeme kwani ukuaji wa matumizi ya umeme umeongezeka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *