USHIRIKIANO WA TANZANIA NA HUNGARY WAZIDI KUNG’ARA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili jijini Budapest, Hungary kwa ya ziara ya kikazi inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya Tanzania na Hungary.
Mara baada ya kuwasili, Waziri Kombo amefanya kikao cha ndani cha maandalizi na timu ya Tanzania kabla ya kukutana na viongozi wa Serikali ya Hungary kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Hungary katika sekta ya maji, elimu na kujengeana uwezo, afya, biashara na uwekezaji, utalii, nishati na mazingira, michezo na utamaduni.


Ziara hiyo ya siku nne inafuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Mhe. Péter Szijjártó. Aidha, Mhe. Kombo ameongozana na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb.); Balozi wa Tanzania nchini Hungary Mhe. Hassani Mwamweta; Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri; Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani, Balozi Swahiba Mndeme; Kamishna wa Fedha za Nje, Bw. Rished Bade na Kamishna wa Madeni, Bw. Japhet Justine kutoka Wizara ya Fedha; pamoja na Mkuu wa Utawala na Fedha wa Ubalozi wa Tanzania Hungary, Mhe. Angela Ngaillo.

