HAPI: CHADEMA NI WAGANGA NJAA, WANATAFUTA HURUMA ZA WAFADHILI KWA KUPIGA KELELE”


Mbulu – Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Ally Hapi (MNEC), ameibuka na kuibonda vikali CHADEMA, akiwashangaa kwa kudai Katiba Mpya ilihali wao wenyewe walikimbia Bunge la Katiba mwaka 2014 jijini Dodoma wakiwa wamejilipa posho za vikao hivyo.
Akizungumza na wananchi wa Mbulu vijijini, Hapi alisema kelele za CHADEMA kuhusu Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi si kwa ajili ya maslahi ya wananchi bali ni njia ya kutafuta huruma ya wafadhili wao wa nje, ambao huwapa fedha kwa masharti ya kueneza vurugu na kudai mabadiliko ya kisiasa.

“Wanajua bila kupiga kelele na kutangaza machafuko, wafadhili wao hawatatoa pesa. Huu ni uhuni wa kisiasa, na wananchi wanapaswa kuwa makini wasidanganywe,” alisema Hapi huku akishangiliwa.
Aidha, aliwashangaa viongozi wa CHADEMA wanaopinga Tume ya Uchaguzi ilhali ni hiyo hiyo iliyowapitisha baadhi yao kuwa wabunge wa majimbo mwaka 2015. “Leo wanabeza Tume hii, lakini walipotangazwa washindi walishangilia. Je, sasa ni mbaya kwa sababu tu hawaoni nafasi ya kushinda?” alihoji.

Kwa upande mwingine, Hapi alizidi kuhoji uwezo wa CHADEMA kwa kushindwa hata kusimamisha wagombea wa kutosha kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, ambapo kati ya nafasi zaidi ya elfu 80, waliweza kusimamisha wagombea kwa asilimia 30 tu.
“Kama chama kinashindwa hata kusimamisha wagombea wa serikali za mitaa, watawezaje kushinda na kuongoza nchi? Hii ni dalili tosha kuwa hawana mtandao wala ushawishi kwa wananchi,” alisisitiza.
Hapi aliwataka wananchi waendelee kuamini CCM, chama chenye mtandao imara na kilicholeta maendeleo makubwa nchini badala ya kudanganywa na wapiga kelele wasiokuwa na mipango ya kweli ya maendeleo.
