BARABARA NJIA NNE NA SITA KUJENGWA JIJINI DODOMA

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imepanga kupanua Barabara za kuingia na kutoka katikati ya jiji la Dodoma zenye jumla ya urefu wa kilometa 220 kwa kuzijenga kwa njia nne na sita kwa lengo la kuhakikisha jiji la Dodoma linaondokana na msongamano wa magari na kusaidia kuboresha huduma za usafiri na uchukuzi.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Mipango na Miundombinu wa TANROADS, Mhandisi Ephatar Mlavi wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akielezea Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha Miaka minne inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Februari 17, 2025 katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO.
Mhandisi Mlavi amezitaja barabara hizo kuwa ni Barabara ya Dodoma – Morogoro ambayo itajengwa (km 70), Dodoma – Arusha (km 50), Dodoma – Singida (km 50) na Dodoma – Iringa (km 50).
“Nia ni kuhakikisha barabara hizi zinaungana kwa urahisi na barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma ‘Dodoma Outer ring Roads’ na hivyo kulifanya jiji la Dodoma kuwa la mfano lisilo na msongamano wa magari na hivyo kuvutia shughuli za ukuaji wa uchumi”, amesema Mhandisi Mlavi.
Mhandisi Mlavi amefafanua kuwa upanuzi wa barabara hizo utatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na utekelezaji wake utaanza na barabara zinazoingia na kutoka katika jiji la Dodoma kuelekea Chamwino (km 32), barabara ya Dodoma kuelekea Iringa- Mkonze (km 4.5) na barabara ya Dodoma kuelekea Arusha – Zamahero (km 8.5).
Aidha, Mlavi ameeleza kuwa hadi kufikia Februari, 2025 utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya mzunguko (km 112.3) sehemu ya kwanza ya Nala – Veyula – Mtumba – Ihumwa Bandari Kavu (km 52.3) umefika asilimia 91 na sehemu ya Pili ya Ihumwa – Bandari Kavu – Matumbulu – Nala (km 62) umefika asilimia 85.
Mlavi ameongeza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kupunguza msongamano katika miji na majiji mengine ikiwemo mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Mwanza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewapongeza wahandisi wote wa TANROADS nchini kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha miradi ya barabara, madaraja, na viwanja vya ndege inatekelezwa vizuri ili kuleta tija kwa Taifa.
Katika kipindi cha Awamu ya Sita kuanzia mwaka 2021 hadi Februari 2025, Serikali kupitia TANROADS imepata mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege nchini ambapo barabara zenye urefu wa jumla ya KM 15,625.55 zimekuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji, madaraja makubwa tisa (9) yamekamilika kujengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 381.301 na madaraja kumi (10) yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.