WANANCHI WA MARA KUNUFAIKA NA MIFUMO KUPITIA COPRA
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi amewataka wananchi wa mkoa huo kuwa tayari kunufaika na fursa nyingi za kiuchumi zilizo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao kupitia matumizi ya mifumo ya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko.
Mhe. Mtambi ameyasema hayo leo tarehe 22 Januari 2025 wakati Mkutano wa wadau wa Mazao ya Choroko na Dengu mkoani Mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bi. Irene Mlola kuwasilisha mwongozo wa kitaifa wa biashara ya mazao ya Dengu, choroko,mbaazi, soya na ufuta.
Mhe. Mtambi amesema uwepo wa mifumo ya stakabadhi za ghala pamoja na minada ya mazao ya kidigitali itawasadia wakulima kupata bei nzuri na kuwaepusha na kuuza kwa bei zisizo za faida na kudhulumiwa kwenye vipimo.
Awali akitoa wasilisho la mwongozo wa kitaifa wa biashara ya mazao ya dengu, choroko,mbaazi, soya na ufuta, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Bi. Irene Mlola amesema kupitia mifumo ya mauzo ya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko wakulima watakuwa huru kwenye kuamua bei itakayowapa maslahi ya kiuchumi kwa kuzingatia thamani ya mazao yao na vipimo sahihi.
Mkurugenzi Mlola ameongeza kuwa COPRA imejidhatiti kuhakikisha kuwa biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko inafanyika kwa kuzingatia uwazi na haki , hivyo basi vibali vya usafirishaji wa mazao ya dengu, mbaazi, choroko, soya na ufuta vitatolewa kwa wanunuzi waliosajiliwa na walionunua mazao hayo kupitia mifumo iliyoelekezwa na serikali.