ULEGA AZINDUA AZAM SEA TAXI, AWATAKA WAVUVI KUTOTUPA NYAVU HOVYO
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amewataka wananchi wanaojishughulisha na uvuvi maeneo ya Kigamboni kutunza mazingira na kutotupa nyavu katika njia inayopita vivuko ili viweze kutoa huduma ya kuvusha wananchi kwa ufanisi na ubora.
Ulega ametoa agizo hilo leo Januari 23,2025 jijini Dar es Salaam wakati akikagua na kuzindua vivuko viwili vitakavyofanya safari za Magogoni – Kigamboni vinavyomilikiwa na Kampuni ya Azam ambavyo vitapunguza adha ya usafiri kwa wakazi Dar es Salaam hususan wananchi wa maeneo ya Kigamboni.
“Naomba niwasisitize ambao wanatumia maeneo haya kufanya shughuli zao za uvuvi, ni vizuri tuwe na utaratibu wa kutazama maeneo haya [Kigamboni] ili shughuli zingine zisiingiliane na njia za vivuko kwa sababu vimekuwa vikipata changamoto na kuharibika”- amesema Ulega.
Aidha Ulega amesema vivuko hivyo vitapunguza adha kwa wananchi wanaosubiria kivuko kwa zaidi ya saa moja na badala yake sasa watatumia dakika tano kuvuka huku kivuko kimoja kikiwa na uwezo wa kubeba abiria 200 – 250 kwa wakati mmoja.
“Mtanzania wa hapa Kigamboni aliyekuwa anakaa saa nzima akisubiri kivuko, historia inaandikwa hatatumia muda huo tena atakuwa yeye anasubiriwa na kivuko, kivuko kimoja kitakwenda kubeba mpaka watu 2500 kwa saa moja”- ameongeza Ulega.
Ulega amewahakikishia wananchi kuwa vivuko hivyo ni salama, vimekaguliwa na kupata Ithibati ya kuwasafirisha abiria na kuwataka TEMESA, TASAC na AZAM MARINE kuendelea kushirikiana kuhakikisha usalama wa wananchi wanaotumia vivuko unazingatiwa wakati wote.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Selemani Kakoso ameipongeza Serikali kwa kuendelea kushirikiana na Sekta binafsi katika kutoa huduma kwa wananchi, na kuiomba Kampuni ya Azam Marine kuwekeza katika maeneo mingine ikiwemo Ziwa Victoria ili waweze kupata wigo mpana wa kutoa huduma kwa wananchi.
“Ni vema Azam Marine waangalie na uwezekano wa uwekezaji ndani ya ziwa Victoria na tunahitaji kuwakuza hawa wawekezaji wa ndani na nikuombe Mheshimiwa Waziri tuhakikishe tunapopata fursa tutumie wakandarasi wa ndani kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi yetu”.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema vivuko hivyo vitasaidia kurahisisha usafiri kwa wananchi wa Kigamboni – Magogoni na jambo la kusingizia muda linakwenda kuisha.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro Kilahala amesema kwa sasa Mv Kigamboni na Mv Magogoni vipo kwenye matengenezo makubwa hivyo kituo kimebaki na kivuko cha Mv Kazi ambapo katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali imeingia ubia na Kampuni ya Azam Marine ili kutoa huduma ya kusafirisha abiria Magogoni – Kigamboni.
Ushirikiano wa TEMESA na AZAM Marine ambao unatarajiwa kuwa na Sea Taxi 8 utaboresha huduma katika eneo hilo ambalo huvusha takribani abiria 70,000 kwa siku.