WAKAZI ZAIDI YA 1,000 MPIJI MAGOE KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MAJISAFI

0

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji Mpiji Magoe katika kata ya Mbezi Wilayani Ubungo wenye lengo la kutatua adha ya maji na kuhudumia kaya takribani 1,000

Akizungumza utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi msimamizi wa mradi, Agness Kenani amesema mradi wa maji Mpiji Magoe unaotekelezwa kwa gharama ya Shilingi Milioni 877 unakwenda kujibu changamoto ya maji katika eneo hilo lililokuwa halina mtandao wa Maji DAWASA.

“ Utekelezaji wa mradi huu umeanza mwezi Agusti, 2024  na unajumuisha uchimbaji na ulazaji wa bomba za ukubwa wa inchi 8 na inchi 6 kwa umbali wa Kilomita 7, kazi hii mpaka sasa ipo zaidi ya asilimia 25 na kazi zinaendelea kwa kasi” alifafanua.

Mhandisi Agness amesema baada ya mradi kukamilika Wananchi wa eneo hilo watasahau matumizi ya maji chumvi yatokanayo na visima na watakua na uhakika wa Majisafi na salama.

Kwa upande wake, Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Mpiji Magoe, Honest Peter amewashukuru DAWASA kwakuwa wasikivu na kuja na suluhisho la huduma ya maji kupitia mradi huu.

“Tulipofikisha mahitaji yetu DAWASA, wamekuwa wasikivu na kutoa ushirikiano, leo tunaona mradi unatekelezwa kwa kasi na tumeshapokea sehemu ya mabomba kwajili ya mradi huu,” amesema Honest

Honest amesema eneo la Mpiji walisumbuka na huduma ya maji kwakua eneo kubwa halikua na mtandao wa DAWASA, lakini sasa wananchi wana matumaini makubwa ya kupata huduma bora ya majisafi.

Esther Daudi, mkazi wa mtaa wa Mpiji Magoe amepongeza jitihada zinazofanyika kuwapatia huduma ya majisafi wananchi wa eneo hilo na kuomba mradi utekelezwe kwa kasi zaidi ili uweze kuleta tija kwa wakazi wa eneo hilo na kufurahia huduma ya majisafi.

Mradi wa maji Mpiji Magoe utanufaisha wakazi wa maeneo ya Machimbo, Mpiji Centre, Mpiji CCM, Masaki Ndogo, Bedisaida, Kwa Mzungu pamoja na Torino huku ukienda kuhudumia wateja zaidi ya 1,000 kwa kuwapatia huduma bora ya majisafi na salama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *