TMA YAWAPIGA MSASA WANAHABARI WA TAARIFA ZA HALI HA HEWA

0

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wanahabari nchini kuzingatia miongozo ya utoaji wa taarifa za hali ya hewa pamoja na kuongeza ubunifu na ufanisi katika kuandaa taarifa hizo kwa kushirikiana na wataalamu ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 22, 2025 jijini Dar es Salaam katika warsha ya kuwajengea uwezo kuhusu utabiri wa msimu wa mvua za masika 2025, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (PCC) Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa wanahabari wanapaswa kutoa taarifa sahihi ili kufikia malengo na kuleta tija kwa Taifa.

“Tuendelee kuelimisha jamii, kuwa na uthubutu, ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kufikisha taarifa, kufanya hivyo mnasaidia kuokoa maisha ya watu kwa kuepukana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa ” amesema Dkt. Chang’a

Katika hatua nyengine ameeleza kuwa mwaka 2024 kulikuwa na ongezeko la joto duniani 1.55 na kuvunja rekodi, huku nchini Tanzania takwimu zinaonesha kulikuwa na ongezeko la joto 0.7.
“Kila mwaka joto linaendelea kuongezeka hali ambayo inatokana na changamao ya uwepo wa hali ya mbaya ya hali ya hewa ikiwemo uwepo wa vimbunga” amesema Dkt. Chang’a.

Dkt. Chang’a ameishukuru Serikai ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya hali ya hewa, kwani mwaka 2024 walifanikiwa kununua rada mbili ambazo zimefungwa Mkoa wa Kigoma na Mbeya na kuifanya Tanzania kuwa Nchi pekee Afrika ya Mashariki katika kuwa na vifaa bora vya hali ya hewa.

Meneja wa Ofisi Kuu ya Utabiri TMA Dkt. Mafuru Kantamla, amesisitiza umuhimu kwa wanahabari kufanya kazi kwa kuzingatia uweledi, maadili pamoja na kuendelea kuwa na nidhamu katika kuhabarisha jamii kuhusu taarifa za hali ya hewa.

Nao wanahabari wameishukuru TMA kwa kuendelea kuwajengea uwezo wa kuandaa taarifa za hali ya hewa ambazo zimeweza kuisaidia jamii na wadau mbalimbali kujitayarisha na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mwandishi wa habari wa Kiss Fm Bw. Mussa Khalid, amesema kuwa taarifa za hali ya hewa zimekuwa na manufaa makubwa kwa jamii hasa katika kuzuia majanga na kusaidia kutekeleza mipango ya serikali..’’Wanahabari tunatambua juhudi za TMA katika kuboresha ushirikiano na utoaji wa taarifa za kisayansi kwa umma”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *