MKURUGENZI WA WHO ATEMBELEA KITUO CHA AFYA MAKOLE
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo Januari 20, 2025 ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) DKt. Tedros Ghebreyesus kukagua huduma za afya ya mama na mtoto (CEMOC) katika Kituo cha Afya Makole Mkoani Dodoma.
“Tumekuja hapa katika Kituo cha Afya Makole na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros Ghebreyesus kwa lengo la kuona juhudi za Serikali za kuhakikisha tunaokoa vifo vya mama na mtoto lakini pia miradi ambayo Serikali inaendelea kuisimamia,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amesema huduma za msingi ambazo zinatolewa katika kituo hicho ni pamoja na huduma ya uzazi mama na mtoto ili kuendelea kuokoa vifo vya mama na mtoto kwani hadi sasa Serikali imepunguza vifo hivyo kutoka 556 kwa vizazi hai 100,000 hadi 104 kwa vizazi hai 100,000 ndani ya miaka minne.