SERIKALI YA TANZANIA INAENDELEA KUISHUKURU IMF – DKT. NATU
Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El Maamry Mwamba, amekutana na kufanya mazungumzo na Tukubya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ikiwa ni sehemu ya ziara ya timu hiyo kufanya tathimini ya ushirikiano katı ya Tanzania na IMF.
Akizungumza katika kikao maalum kilichofanyika jijini Dodoma, Dkt. Mwamba alisema kuwa ziara hiyo ya Tiku ya Wataalam kutoka IMF inalenga kujadili maendeleo ya hivi karibuni na matarajio yanayohusiana na sera za uchumi na bajeti pamoja na maendeleo ya programu za ECF na RSF.
Alilipongeza na kulishukuru Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwa ushirikiano inalotoa kwa Serikali ya Tanzania huku akiahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia vyema fedha za maendeleo zinazotoleww na Shirika hilo na kufikia lengo yakiyokusudiwa.
“Serikali ya Tanzania inaendelea kushukuru msaada wa kipekee wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) katika kutoa mkopo wa masharti nafuu chini ya Mpango wa Mikopo wa Masharti Nafuu (ECF), Serikali ya Tanzania inaendelea kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa,’’ alisema Dkt. Mwamba.
Aliongeza kuwa Tanzania inaendelea vyema kufikia malengo ya mpango wa ECF, kwa kuwa Viashiria vya Utendaji (QPCs) na Vipengele vya Kimuundo (SBs) vya Desemba 2024 vitafikiwa
Kwa upande wake Kiongozi wa Msafara kutoka IMF, Idara ya Afrika, Bw. Charalambos Tsangarides, alisema kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kukuza uchumi IMF itaendelea kutoa ushirikiano na kuiunga mkono Tanzania ili ifikie malengo yake ya kiuchumi.
‘’Inafurahisha sana na kwa kweli inatia moyo kuendelea kuwa nanyi na tunaona juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania, sisi kama IMF tutaendelea kushirikiana nanyi katika kila hatua’’ alisema Bw. Tsangarides.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Shaaban, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmannuel Tutuba, Kiongozi wa IMF Idara ya Afrika, Bw. Charalambos Tsangarides, Mwakilishi Mkazi wa IMF, Bw. Sebastian Acevedo, Wafanyakazi wa IMF pamoja na Maafisa wengine wa Serikali ya Tanzania