NDEJEMBI AZUIA UENDELEZWAJI WA ENEO LENYE MGOGORO SUMBAWANGA

0

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Mwekezaji wa Shamba la Malonje lililopo katika Kijiji cha Sikaungu Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa kutoendeleza eneo ambalo lina mvutano kati ya mwekezaji huyo na wananchi wa kijiji hiko.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo Januari 14, 2025 kwenye mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kijiji cha Sikaungu alipofika kutatua mgogoro huo uliodumu kwa miaka 13.

“ Nafahamu mgogoro huu umedumu kwa muda mrefu lakini niwahakikishie hakuna kisichowezekana, ni lazima kupata suluhu. Hivyo nimtake Mwekezaji wa Shamba hili la Malonje kutoendeleza upandaji wa mazao ya kudumu lakini pia na wananchi msiingilie shamba hili hadi suluhu itakapopatikana.

Lakini pia nimuelekeze Kamishna wa Ardhi kutuma timu ya wataalamu kutoka Wizarani kuja hapa Sikaungu kupitia upya mipaka yote ya shamba hili na kuona ukubwa wake na uhalisia wa vipimo vilivyopo, kazi hii ifanyike ndani ya siku 14 ili tuweze kupata ufumbuzi wa jambo hili mapema,” Ameelekeza Mhe. Ndejembi.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kwala na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameishukuru Serikali kwa hatua kubwa inayoendelea kuchukua katika kutatua mgogoro huo ili wananchi na mwekezahi waweze kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao kwa amani.

Katika ziara hiyo, Mhe Waziri Ndejembi ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Nyakia Chirukile pamoja na timu ga wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiwemo, Kamishna wa Ardhi Bw. Mathew Nkhonge.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *