WANANCHI VIJIJINI WAHIMIZWA KUTUMIA UMEME KUJILETEA MAENDELEO
Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mhe. Mohamed Mtulyakwaku amewataka wananchi waliofikiwa na miradi ya umeme vijijini kuhakikisha wanaunganisha nyumba zao na umeme kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Mhe. Mtulyakwaku ametoa rai hiyo wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mabama, wilayani Uyui Mkoa wa kwa lengo la kutoa elimu kwa umma na kuhamasisha wananchi kuunganisha umeme.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imetumia gharama kubwa kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji vyetu. Hivyo nitoe rai kwa wale wote ambao miundombinu hii imewafikia karibu na nyumba zenu mhakikishe mnaunganisha umeme katika nyumba zenu,” amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Mhe. Mtulyakwaku pia amesema wananchi Wana jukumu la kulinda miundombinu hiyo ya umeme na kuwataka wanapoandaa mashamba kwa ajili ya kilimo waepuke kuchoma moto nguzo za umeme.
“Nawasihi mtumie umeme huu kujiletea maendeleo ya kiuchumi ili kutimiza dhamira ya Serikali kusambaza umeme vijijini. Mnaweza kufungua shughuli mbalimbali kama saluni, sehemu za kuonyesha mipira, kuuza vinywaji baridi,” amesema Mhe. Mtulyakwaku.
Kwa upande wake Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Tabora, Mha. Oscar Migani amewahakikishia viongozi pamoja na wananchi kuwa miradi yote inayotekelezwa na REA itakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.
Mha. Migani amesema kuwa vijiji vyote 156 vya Wilaya ya Uyui vimefikishiwa umeme na vitongoji 468 kati ya vitongoji 706 tayari vina umeme.