WANANCHI WAMPONGEZA RAIS SAMIA KUFIKISHA UMEME VITUO VYA AFYA VIJIJINI
Wananchi katika Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora wamempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha umeme kwenye vituo vya afya vijijini.
Wamesema kuwa kufika kwa umeme kwenye vituo vya afya vijijini kumeboresha huduma za afya ambapo awali walilazimika kusafiri kwenda umbali mrefu au kusubiri siku nyingi kupata majibu ya vipimo vyao ambavyo vilipelekwa hospitali za mjini.
“Tulikuwa ukipata shida unatakiwa uende Lolangulu, Ndono au uende Usoke. Vifo vya akina mama vitapungua kwa sababu huduma tunaipata karibu. Ilikuwa mtoto akipata dharura ya haraka ulitakiwa upande gari uende mjini mpaka Kitete. Hauna nauli ya haraka inakuwa changamoto, tulikuwa tunapoteza watoto wetu. Tunakushkuru sana Mama Samia Suluhu,” amesema Mariam Haruna mkazi wa Kijiji cha Mabama Wilaya ya Uyui mkoani Tabora.
Mzee Omary Mohammed na Suleiman Mrisho pia wamemshkuru na kumpongeza Mhe. Rais, Dkt. Samia kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo miradi ya nishati ya umeme katika vijiji vyao na kuahidi kutumia uwepo wa umeme kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Hassani Mwakasuvi kilichopo Kijiji cha Mabama, Dkt. Renatus Mathias amesema uwepo wa umeme katika kituo hicho umewezesha kuboresha huduma za afya na kuweza kutoa majibu kwa haraka kwa wananchi.
“Kuna vifaa tulikuwa hatuwezi kuvitumia awali sababu vinatumia umeme hivyo wananchi walilazimika kwenda kufanya vipimo nje ya kituo chetu. Lakini kwa sasa vifaa vyote vinafanya kazi na tunafanya vipimo na majibu tunatoa hapahapa. Hatuna haja ya kusafirisha vipimo wilayani au mkoani kwa ajili ya kupata majibu na hivyo wagonjwa wanatibiwa kwa wakati,” amefafanua Dkt. Mathias.
Akizungumzia mradi huo wa kupeleka umeme kwenye vituo vya afya na pampu za maji unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka REA, Jaina Msuya amesema kuwa mradi huo wa kupeleka umeme kwenye vituo vya afya na pampu za maji umelenga kuboresha sekta ya afya vijijini.
“Katika kuendelea kuboresha maisha ya wananchi wake, Serikali ya Awamu ya Sita imejenga vituo vya afya katika ngazi ya kata na vituo hivyo vingi vimeshafikishiwa huduma ya nishati ya umeme. Na vinawezesha wananchi kupata huduma bora kabisa ya afya,” amefafanua Msuya.