ARUSHA MBIONI KUFANYWA KUWA KITOVU CHA UTALII WA MATIBABU UKANDA WA AFRIKA MASHARIKI
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda na Waziri wa Afya nchini Tanzania Mhe. Jenista Mhagama, wamekubaliana kukutana Dodoma Makao Makuu ya Wizara hiyo, kufanya mazungumzo ya pamoja ya kupanga utekelezaji wa ndoto na Maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuufanya Mkoa wa Arusha kuwa Kitovu cha Utalii wa Matibabu kwa Ukanda wa Afrika ya Mashariki.
Wakati wa Mazungumzo yao Makao makuu ya Mkoa Jijini Arusha, Mhe. Makonda amemueleza Waziri Mhagama kuwa Mkoa unatekeleza kwa kasi agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan la kukuza utalii wa aina mbalimbali Mkoani hapa, akisema kupatikana kwa Hospitali itakayokuwa na Huduma za kibingwa na Kibobezi sambamba na madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya nchi, kutasaidia kuwavuta watu wanaoizunguka Tanzania na Raia wa kigeni kusafiri kufuata matibabu hayo Mkoani Arusha na hivyo kukuza utalii na kusisimua pato la Mkoa wa Arusha.
Waziri Mhagama, Kando ya Kumshukuru Mhe. Makonda kwa kusimamia vyema utoaji huduma za kiafya Mkoani Arusha ikiwemo Programu ya Kliniki yake ya afya iliyofanyika mwaka 2024, amemuahidi kuwa atamuita Jijini Dodoma, kujadiliana pamoja Mkakati madhubuti wa kutekeleza maono ya kujenga Hospitali mpya ya kibingwa ama kuiongezea uwezo Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru ili kukidhi viwango vinavyohitajika Kimataifa.
Aidha wawili hao Katika mazungumzo yao leo Januari 10, 2025, wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika kutimiza dhamira ya Rais Samia katika kuwapatia wananchi huduma bora za kiafya, ambapo Waziri Mhagama amesema Wizara yake pia ipo mbioni kuupatia Mkoa wa Arusha mashine mpya ya MRI kama sehemu ya maboresho ya utoaji wa huduma za kiafya Mkoani hapa na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa mashine hiyo muhimu kwa matibabu mbalimbali.