LISSU ATHIBITISHA USHIRIKI WA FR. CHARLES KITIMA KWENYE VIKAO VYA SIRI VYA CHADEMA
Katika tukio lililotokea leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, amethibitisha hadharani kuwa Fr. Charles Kitima, Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alihudhuria vikao vya siri vya chama hicho vilivyofanyika katika ukumbi mdogo wa Macapuchino ulioko eneo la kanisa, Msimbazi Centre, jijini Dar es Salaam.
Mwanzoni mwa mwezi Desemba, taarifa za ndani zilisambaa zikidai kuwa Fr. Kitima, kiongozi wa juu wa Kanisa Katoliki, alihusishwa moja kwa moja na vikao vya CHADEMA. Taarifa hizo zilizua mijadala mitandaoni, huku baadhi ya wadau wakitilia shaka ukweli wake na wengine wakihoji nafasi ya kiongozi huyo wa kidini katika siasa za vyama. Hata hivyo, leo Lissu amekiri waziwazi ushiriki huo, akiondoa shaka kuhusu madai hayo ambayo awali yalionekana kama uzushi.
Ukaribu wake na Fr. Kitima unatokana na ukweli kwamba wote wanatoka kijiji kimoja mkoani Singida. Ukaribu huu, kulingana na vyanzo vya karibu, umesababisha Fr. Kitima kuwa mmoja wa wapangaji wakuu wa mikakati ya kampeni za Lissu na hatua za kuipinga serikali.
Uthibitisho huu umetajwa kama “kuvuliwa nguo kwa kanisa,” huku baadhi ya wadau wakidai kuwa hatua ya Lissu kufichua ushiriki wa Katibu wa TEC katika siasa za vyama imeweka wazi mgongano wa maadili unaohusiana na nafasi ya viongozi wa dini katika masuala ya kisiasa.
Kanisa Katoliki linatakiwa kutoa tamko rasmi kufuatia kauli ya Lissu, ingawa mjadala mkubwa umeibuka mitandaoni, huku waumini na wadau wa siasa wanakosoa hatua hiyo kama kinyume na maadili ya kidini.
Tukio hili linaongeza mvutano kuhusu nafasi ya viongozi wa dini katika siasa za Tanzania.