DC KINONDONI APONGEZA NHC KWA UBUNIFU KATIKA UJENZI WA MRADI WA MOROCCO SQUARE

0

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amefanya ziara katika Mradi wa Morocco Square, unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Morocco, jijini Dar es Salaam. Ziara hiyo ililenga kukagua maendeleo ya mradi huo mkubwa ambao unalenga kuboresha makazi na kukuza mazingira ya kibiashara katika Wilaya ya Kinondoni.

Akiwa kwenye eneo la mradi, Mkuu wa Wilaya amepongeza juhudi za NHC kwa kuwekeza miradi mikubwa inayoongeza thamani ya maeneo na kuboresha maisha ya wakazi wa Kinondoni. “Tunawashukuru kwa ubunifu katika ujenzi, na hasa kwa miradi hii ambayo imeongeza thamani kubwa kwa maeneo yetu. Tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba biashara zinafanyika vizuri na huduma zinaendelea kusogezwa karibu na wananchi,” alisema Mtambule.

Aidha, Mtambule alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza juhudi za kukwamua miradi mikubwa iliyokuwa imekwama, ikiwemo Samia Housing Scheme na Kawe 711, ambayo sasa inaendelea kwa kasi na kufikia viwango vya juu.

Mkuu wa Wilaya alieleza kuwa mradi wa Morocco Square umekaribia kukamilika kwa asilimia kubwa, na ameelekeza kwamba hatua zilizobaki, ambazo ni asilimia 2 pekee, zikamilishwe haraka ili biashara zianze.

“Ninashauri ubunifu huu wa NHC usiishie hapa Morocco pekee. Shirika liangalie pia maeneo mengine kama Bunju, Madale, na Mabwepande, ambako kuna fursa nyingi za uwekezaji, ikiwemo uuzaji wa viwanja,” aliongeza.

Kwa upande wake, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa ushauri wake na ushirikiano anaouonyesha mara kwa mara. Wamesisitiza dhamira yao ya kuendelea kuleta maendeleo kupitia miradi ya makazi bora na huduma zinazokidhi mahitaji ya Watanzania.

Mradi wa Morocco Square unaendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za NHC za kukuza uchumi wa maeneo ya mijini, kuboresha maisha ya wakazi, na kuimarisha sekta ya ujenzi nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *