COPRA KUWEZESHA WANANCHI KUNUFAIKA NA MAZAO YA NAFAKA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko COPRA Bi. Irene Mlola ametembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Stephen Ndaki.
Mkurugenzi Mkuu Bi. Mlola amempa taarifa Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Ndaki kuwa COPRA imeanzisha ofisi za kanda ikiwemo Kanda ya Ziwa ili kurahisisha huduma za Mamlaka kwa wananchi na wadau wote walio kwenye mnyororo wa thamani katika mazao.
Mkurugenzi Mlola amemueleza Katibu Tawala wa Mkoa kuwa COPRA itashirikiana na Ofisi za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wananchi wananufaika na mavuno ya mazao yao hasa Nafaka na Mazao mengine mchanganyiko.
Aidha Mkurugenzi Mkuu wa COPRA ameongeza kuwa kwa mkoa wa Kagera Ofisi za COPRA zipo ndani ya Chuo cha Kilimo cha Wizara ya Kilimo ( MATI) Maruku kilichopo Manispaa ya Bukoba.
Maafisa wa COPRA watashirikiana na wataalamu wote wa kilimo kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji katika kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Stephen Ndaki amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa COPRA na kumuahidi ushirikiano ili malengo ya Serikali ya kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara wa mazao kiuchumi yatimie.