ULEGA ATOA SAA 72 MAWASILIANO DARAJA LA GONJA MPIRANI YAREJEE
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ametoa saa 72 kwa Wakala ya Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Kilimanjaro kurejesha mawasiliano katika daraja la Gonja Mpirani.
Hatua hiyo inafuatia kuvunjika kwa daraja hilo hivi karibuni kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika safu ya milima ya Pare Wilayani Same.
” Ndugu zangu poleni sana kwa changamoto iliyotokea, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amenituma niwape pole na niwahakikishie ujenzi wa daraja jipya utakamilika ndani ya siku tatu ili muendelee na shughuli zenu kama kawaida”, amesema Ulega.
Amemtaka Mtendaji mkuu wa TANROADS Eng. Mohamed Besta kuhakikisha wataalam kutoka makao makuu wanashirikiana na wa mkoa kufanya kazi usiku na mchana ili mawasiliano ya Ndungu-Maore yarejee.
” Kipimo cha ufanyakazi mzuri wa meneja wa TANROADS itakuwa ni uwezo wake kukabiliana na dharura na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati”, amesisitiza Ulega.
Amezungumzia umuhimu wa mameneja wote wa TANROADS nchini kuchukua tahadhari kuelekea msimu wa mvua za masika ili kuepuka magari kukwama na usumbufu kwa wasafiri.
Naye Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu ameipongeza TANROADS kwa kuchukua hatua za haraka katika kurudisha mawasiliano katika barabara hiyo.
Daraja la Gonja Mpirani liko katika barabara ya Same-Mkomazi Km 105 na linaunganisha kata za Ndungu na Maore.