MIREMBE YAWAITA WATANZANIA KUPATA HUDUMA ZA AFYA YA AKILI
Watanzania wametakiwa kuitumia Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe kupata huduma za matibabu zikiwemo za kibingwa ambazo zinatolewa na wataalam mbalimbali waliopo kwani na Serikali ya awamu ya sita imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu, vifaa tiba na vitendani.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma na Dkt. Godfrey Kayumba Mkama ambaye ni daktari katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, mara baada ya Klabu za Dodoma Jogging kushiriki mazoezi na baadaye kufanya usafi katika hospitali hiyo kwa lengo la kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi na kukabiliana magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya akili, kupunguza msongo wa mawazo pamoja na kuimarisha viungo vya mwili.
“Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa kwa kutupa vifaa tiba vya kisasa na kuboresha miundombinu pamoja na kuongeza wataalamu ili wananchi wapate huduma bora za afya na uwekezaji uweze kuleta tija kwa jamii”, ameeleza Dkt. Mkama.
Aidha, Dkt. Mkama ameongeza kuwa ukiacha kwamba Hospitali hiyo wanahudumia wagonjwa ambao wanakabiliana na magonjwa ya akili, msongo wa mawazo, uraibu wa pombe, bangi na vilevi vingine pia wananchi wanapaswa kuitumia Hospitali hiyo kupata matibabu ya magonjwa mengine kutokana na uwepo wa madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, magonjwa ya Watoto, macho na mifupa ambayo ni nafuu kuliko hata hospitali nyingine hapa nchini kwa kutumia bima au malipo taslimu.
“Mkaribie sana hapa kuna vitengo vya wataalam wa Saikolojia usisubiri uumwe, ukiangalia hivi sasa maisha yetu tunakimbizana hivyo kitu kidogo tuu utahitaji ushauri mfike hapa kuna wataalamu wa saikolojia watawahudumia kwa ufanisi ”, ameeleza hayo Dkt. Mkama
Kwa Upande wake kaimu Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Bakar Abdulrahman ametoa rai kwa wanamichezo wote kutunza afya zao kwa kupunguza matumizi ya wanga pamoja na sukari na kufanya mazoezi na kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwa ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukizwa.
“Nawashukuru wanamichezo wote kwa mazoezi mazuri kwa ajili ya afya zetu kwani kufanya mazoezi mara kwa mara inasaidia kuboresha afya ya mwili na akili”, Amesema Abdulrahman
Naye mwanachama wa Klabu ya Dodoma Fitness, Bi. Zamoyoni Komba, ametoa wito kwa watalaum wa lishe kushirikiana na wanamichezo ili kutoa elimu ya lishe kwa wana michezo na kusaidia kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa jamii. Hata hivyo amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kujiunga na vikundi mbalimbali vya mazoezi ili kulinda afya zao na kundokana na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama sukari na shinikizo la damu.