POLISI YAMSAKA ALIYETANGAZA KUUZA MTOTO KWENYE MITANDAO YA KIJAMII
Jeshi la Polisi limeanzisha msako maalum kumtafuta mtu anayeonekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni akidai kuuza mtoto kwa gharama ya shilingi milioni moja na laki sita. Taarifa rasmi kutoka kwa Jeshi la Polisi inaeleza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mhusika mara baada ya kukamatwa.
Katika taarifa hiyo, Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria za nchi na maadili ya kijamii. Aidha, Jeshi hilo limelaani vikali tukio hilo, likisema kuwa vitendo vya namna hii ni ukiukwaji wa haki za watoto na vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa ustawi wao.
Jeshi la Polisi pia limewataka wananchi kutoshirikiana na kuficha vitendo kama hivi, na badala yake watoe ushirikiano wa dhati kwa vyombo vya usalama ili kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake na kuzuia madhara zaidi kwa watoto wasio na hatia.
Wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia kufanikisha msako huu wametakiwa kuwasiliana na ofisi za polisi kupitia namba za simu zilizotolewa au ofisi za karibu za Jeshi la Polisi.