MKANDARASI ATAKIWA KUONGEZA KASI UJENZI WA MAABARA YA KISASA MIREMBE
Msanifu Majengo kutoka Wizara ya Afya, Seth Silas Akyoo ametoa wito kwa mkandarasi Kiunga Builders kuongeza kasi ya ujenzi wa Mradi wa Maabara ya Kisasa inayojengwa katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe chini ya Ufadhili wa Global Fund kupitia Wizara ya Afya.
Akyoo ametoa wito huo leo Januari 3, 2025 wakati alipofanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Maabara ya Kisasa inayojengwa katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe Jijini Dodoma.
“Nashauri muongeze kasi ya ujenzi ili muweze kukamilisha kwa wakati na nimeona mnaendelea vizuri mpo ndani ya muda kulingana na mpango kazi wa utekelezaji wa mradi huu”, amesema Akyoo.
Akyoo ameongeza kuwa utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Maabara hii ya Kisasa utagharimu kiasi cha shilingi Milioni 800.
Akyoo amesema kuwa maabara hiyo itakapo kamilika itasaidia kuboresha Huduma za uchunguzi katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe na kuleta ufanisi katika Huduma za maabara.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi kutoka Kiunga Builders, Mhandisi Jackson Kitundu amesema wamepokea ushauri waliopewa kutoka Msanifu Majengo kutoka Wizara ya Afya na amehaidi kuufanyia kazi ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kuanza kutoa Huduma kwa wananchi.
“Mradi huu ulianza rasmi Desemba 3 mwaka jana na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 8 ambapo ni Agosti 3, 2025”, ameeleza Mhandisi Kitundu.
Mhandisi Kitundu amesema mpaka sasa toka wameanza ujenzi huo hawajakutana na changamoto yoyote hivyo watahakikisha wanafanya kazi kulingana na mpango kazi uliopo ili kukamilisha mradi huo kwa muda sahihi uliopanga