UJENZI WA BARABARA YA KIMARA – BONYOKWA – KINYEREZI (7KM) WAANZA RASMI
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, amefanya ziara ya kikazi kutembelea barabara ya Kimara – Bonyokwa – Kinyerezi yenye urefu wa kilometa 7, mkoani Dar es Salaam, na kusisitiza umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa barabara hiyo ya kimkakati.
Katika ziara hiyo, Waziri Ulega ameagiza mkandarasi anayejenga barabara hiyo, kampuni ya kizawa ya Nyanza Road Works, kuhakikisha kuwa kazi zinafanyika usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo kwa haraka na kwa ubora unaotakiwa.
“Kazi imeanza rasmi na wananchi wataanza kushuhudia maendeleo ya ujenzi wa barabara hii muhimu. Mkandarasi ahakikishe anakuwa na wafanyakazi wa kutosha na kwa ajira zisizo za ujuzi zitolewe kwa wananchi wa maeneo ya jirani na mradi ikiwemo Bonyokwa kama sehemu ya kurudisha kwa jamii,” amesema Waziri Ulega.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Segerea Bonnah Kamoli, ameunga mkono agizo hilo, akisisitiza kuwa ajira za muda mrefu wakati wa ujenzi ni fursa kwa wananchi wa Bonyokwa, Kinyerezi, Kimara na maeneo jirani.
Barabara hiyo muhimu inatarajiwa kuwa kiunganishi kikubwa kati ya majimbo ya Ubungo na Segerea, hatua inayotarajiwa kuboresha huduma za usafiri na kuinua uchumi wa eneo hilo.
Waziri Ulega ameahidi kuwa serikali itasimamia mradi huo kwa weledi huku akiwahakikishia wakandarasi kuwa malipo yao ni kipaumbele cha serikali.
“Nyanza Road Works mmeonesha rekodi nzuri, tunawaamini, na tunategemea kazi bora zaidi katika mradi huu,” aliongeza.
Wananchi wanaoishi maeneo ambayo barabara hiyo inapita Kimara, Bonyokwa, Kinyerezi na maeneo jirani sasa wana matumaini makubwa ya kupunguza changamoto za miundombinu, usafiri na wanatarajia kunufaika kiuchumi kupitia mradi huu wa ujenzi.
Ujenzi wa barabara hiyo utajumuisha daraja lenye mita 25 na madaraja madogo saba ya kalvati na mkandarasi akitakiwa kufunga taa za barabarani.