TANESCO TEMEKE NA ZECO WAUNGANA KUSHIRIKI MICHEZO KUIMARISHA UMOJA
Timu ya Mpira wa Miguu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke imetoa sare ya bao moja kwa moja na timu ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Disemba 28, 2024. Katika Uwanja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) uliopo Mivinjeni, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa kirafiki ulikuwa na lengo la kuboresha afya pamoja na kudumisha umoja na ushirikiano jambo ambalo litasaidia kuleta tija katika utendaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke Mhandisi Ezekiel Mashola, amesema kuwa kupitia michezo mbalimbali wafanyakazi wataboresha afya zao pamoja na kuendelea kujenga umoja katika kutekeleza shughuli mbalimbali za shirika.
“TANESCO Mkoa wa Temeke tukiwa na timu yetu pamoja na timu ya Shirika la Umeme la Zanzibar tunacheza mechi ya kirafiki kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na kuimarisha Afya” amesema Mhandisi Mashola.
Mhandisi Mashola amesema kuwa ushirikiano huo ni mzuri hivyo mwanzoni mwa mwaka 2025 wanatarajia kwenda Zanzibar kucheza mechi ya kirafiki na ZECO kwa ajili ya kuimarisha mahusiano hayo ambayo yanakwenda kuongeza tija katika utendaji.
Mkuu wa Utawala Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Bw. Hemedi Khamis Nyoni, amesema kuwa lengo la kushiriki michezo na TANESCO Mkoa wa Temeke ni kujenga undugu pamoja na kubadilishana uzoefu.
Nahodha wa timu ya ZECO Nabby Juma pamoja na timu ya TANESCO Mkoa wa Temeke Magesa Juma, wamefurahisha na utaratibu wa shirika kuweka ratiba ya michezo, huku wakieleza kuwa michezo ina faida nyingi ikiwemo kuhamasisha utendaji wa kazi pamoja na kuimarisha mahusiano katika ya Zanzibara na Bara.